TRA yawanoa wahasibu mabadiliko ya mfumo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) ofisi za Geita imewataka wahasibu na wafanyabiashara wa kampuni kufanya kazi kwa kuzingatia maboresho ya mfumo wa uwasilishaji wa ritani za kodi kwa njia ya mtandao.

Ofisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Mkoa wa Geita, Justine Katiti ameeleza hayo Februari 6, 2023 katika semina kwa wahasibu wa makampuni iliyolenga kuwajengea uwezo wa kutuma ritani kutokana na mabadiliko ya mfumo.

Advertisement

Amesema mabadiliko ya mfumo wa mtandao yanatarajiwa kuokoa muda na kuondoa changamoto zilizokuwepo kwa wahasibu na kuboresha ufanisi wa taarifa zinazotumwa TRA kwa ajili ya makadirio ya kodi.

“Maana yake taarifa zitakuwa wazi sasa, kama kulikuwa na taarifa hatuzipati kwa wakati, kupitia huu mfumo tutakuwa tunapata taarifa sahihi.

“Lakini pia kuna taarifa za manunuzi na mauzo, hizi nazo mfumo utakuwa unachukua taarifa wenyewe kutoka kwenye mfumo wetu wa EFD.

“Kwa hiyo uwazi katika masuala ya kibiashara, mauzo na manunuzi, sasa hivi yataweza kuwa wazi na serikali itapata kodi yake na mlipakodi kama ana kodi ya kurejeshewa atarejeshewa kwa usahihi zaidi.”

Mhasibu wa Kampuni ya Elias Chemicals Limited, Christopher Genya ameishukuru TRA na kueleza mfumo mpya utawasaidia kujaza na kutuma mkusanyiko wa taarifa zote muhimu za biashara kwenda TRA.

Mhasibu wa Ofisi ya Askofu, Jimbo katoliki la Geita, Sister Maria Mercy amekiri mfumo mpya utawezesha kutuma taarifa za waajiriwa wengi kwa wakati mmoja zinapohitajika TRA tofauti na hapo awali.

Mhasibu wa Kampuni ya Kamoga, Costantine Evarist amesema mfumo mpya umerahisisha utendaji wa wahasibu hususani katika suala la manunuzi na kuweka taarifa kwa usahihi inapofikia ukaguzi wa TRA.