TRC mguu sawa treni za mizigo SGR

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limekamilisha majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo yatakayotumia reli ya kisasa (SGR) yaliyowasili nchini Desemba mwaka jana.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala ameeleza kuwa majaribio hayo yalifanywa kwa mwezi mmoja yakisimamiwa na usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA).
Taarifa ya Mwanjala jana ilieleza kuwa majaribio hayo yalikuwa na lengo la kuona umadhubuti wa mabehewa, treni inapokuwa kwenye mwendo.
Alieleza kuwa Latra ilikagua mabehewa yote 264 yakiwemo 200 ya kontena na 64 ya mizigo isiyofungwa.
“Latra imejiridhisha kuwa ubunifu wa mwendokasi wa kilometa 120 kwa saa umefikiwa na kuthibitisha kuwa yamefanya vizuri katika mifumo yote muhimu ikiwemo breki na kwenye kona,” alieleza Mwanjala.
Alieleza kuwa Latra imesema itatoa ithibati kwa TRC kwa mujibu wa sheria na kanuni ili mabehewa hayo yaanze kubeba na kusafirisha mizigo.
“Kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 kati ya 1,430 yanayotengenezwa na kampuni ya CRRC ya China ni kiashiria kuwa usafirishaji mizigo katika reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) uko mbioni kuanza,” alieleza Mwanjala.
Desemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema treni ya mizigo itakapoanza, wafanyabiashara wanaweza kusaini mkataba na shirika hilo kuhakikisha mizigo yao inafika kwa muda na siku iliyopangwa.
“Mikataba itasaidia kuwa na uhakika wa kusafirisha mizigo ndani ya siku au saa kadhaa. Tunafahamu kwamba wafanyabiashara wanaisubiri kwa hamu treni hii,” alisema Kadogosa.
Alisema treni ya mizigo itakapoanza hawatachukua mizigo inayobebwa na malori lakini badala yake watajenga bandari kavu ambayo itakuwa kituo cha kushusha mizigo hiyo na malori kuipeleka katika maeneo husika.
Kadogosa alisema badala ya kuendesha lori kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda watakuwa na kituo Isaka ambako treni itashusha mizigo, kisha malori yaisafirishe kwenda Rusumo hadi Kigali.
Alisema treni ya mizigo itapunguza gharama za mafuta yanayotumiwa na malori, kutumia muda mrefu njiani, kuharibu miundombinu na kusababisha ajali. Alisema wenye viwanda watasafirisha mizigo kwa urahisi.
Akieleza SGR inavyovutia uwekezaji, alisema, “Kwala kuna mwekezaji ana viwanda zaidi ya 200 na anapotangaza fursa zake kuita wawekezaji, hueleza kwamba viwanda vipo karibu na reli ya SGR hivyo kurahisisha usafirishaji.”
Kadogosa alisema lengo la serikali limekuwa kuunganisha reli hiyo na nchi za Uganda na Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Awali, Kadogosa alisema SGR itakuwa na manufaa zaidi kiuchumi kwa kusafirisha mizigo na si abiria.
“Unajua treni ni mizigo, abiria haturudishi gharama kwa asilimia 100, sisi akili yetu ipo kwenye mizigo zaidi kuliko kwenye abiria, abiria ni huduma, pesa yetu ipo kwenye mizigo. Tunajenga reli ya kwenda Msongati, pale Msongati kuna machimbo yale ya Nickel,” alisema.



