SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limejipanga kusafirisha abiria milioni sita mwaka 2025/2026 na hadi sasa wamesafirisha abiria milioni 2.1.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema hayo akizungumza katika mkutano wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli na Shughuli zinazohusiana na Reli (RAWUTA).
Kadogosa alieleza kuwa katika mwaka 2025/2026, TRC inatarajia kusafirisha asilimia 10 ya Watanzania, sawa na milioni sita.
“Mpaka jana tulikuwa tumesafirisha abiria milioni 2.1. Tunakwenda vizuri na baada ya kukamilika kwa miundombinu yote, tutasafirisha abiria zaidi,” alisema Kadogosa.
Pia, alibainisha kuwa hivi karibuni walipata kibali cha kupandisha madaraja kwa watumishi 750 kwa mserereko
na watumishi 60 wamepanda cheo kimoja kimoja.
“TRC tunajivunia mwaka wa 10 sasa bila mgomo,” alieleza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete alisisitiza mchango wa vyama vya wafanyakazi katika mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita hasa katika kuimarisha miundombinu ya reli, ni muhimu.
Alisema serikali imejizatiti kutekeleza miradi ya kimkakati, ikiwamo Reli ya Kisasa (SGR) ambayo kipande cha Dar es Salaam – Makutupora (kilometa 722) kilikamilika na huduma ya kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma ilianza kutolewa rasmi mwishoni mwa Juni, 2024.
Alifafanua kuwa manufaa yaliyopatikana ni kupunguza muda wa kusafiri, kuongeza tija katika biashara na uchumi kwa ujumla.