Trump akana kubatilisha matokeo uchaguzi 2020

RAIS wa 45 wa Marekani, Donald Trump amekana mashtaka ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020 nchini Marekani.

Trump alitokea kwa mara ya kwanza jana mahakamani hapo ambapo alisema: “Unapoangalia kile kinachotokea, haya ni mateso ya mpinzani wa kisiasa, hii haikupaswa kutokea Amerika”.

Trump aliomba kesi hiyo inayoskilizwa katika Mahakama ya Barrett Prettyman ya huko Washington, DC kusikilizwa siku nyingine na hakimu alikubali kesi hiyo kusikilizwa tena Agosti 28.

Advertisement

Trump anashtakiwa ikiwa ni siku mbili tu baada ya waendesha mashtaka wa Marekani kuwasilisha mashtaka manne dhidi ya Trump, wakimtuhumu mwanasiasa huyo wa chama cha Republican kutaka kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020 ambao alishindwa na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden.

Kesi hiyo ni ya tatu kufunguliwa mashtaka ya jinai dhidi ya rais huyo wa zamani tangu Machi.

Trump pia anakabiliwa na mashtaka ya serikali huko New York juu ya madai ya malipo ya kimya kimya kwa nyota wa filamu na mashtaka ya serikali yanayohusiana na tuhuma kwamba alishughulikia vibaya hati za serikali huko Florida.

Trump amekanusha makosa yote na kudai kuwa mashtaka hayo ni majaribio ya kuvuruga kampeni yake.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *