TSN, Kituo cha utamaduni Iran kushirikiana biashara

DAR ES SALAAM – Ujumbe kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) umetembelea Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jijini Dar es Salaam kama sehemu ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano wa pande zote mbili.
Ujumbe huo ulihusisha wajumbe kutoka Idara ya Biashara na Uhariri na umetembelea Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapa nchini Tanzania.

Idara ya Biashara, iliongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Bw. Felix Mushi, huku upande wa Uhariri ukiwakilishwa na Meneja wa Huduma za Habari za Kidijitali, Bw. Sylivester Domasa; pamoja na wawakilishi wengine kutoka kitengo cha Mauzo na Masoko.
SOMA ZAIDI

Ujumbe huo ulipokelewa na Mshauri wa Masuala ya Utamaduni kutoka Ubalozi wa Iran na Mkurugenzi wa Kituo hicho cha Utamaduni, Dk. Mohsen Maarefi.

Katika mazungumzo yao, pande zote mbili zilijadili maeneo ya ushirikiano wa baadaye, huku wakikubaliana kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja za kubadilishana utamaduni na kukuza maendeleo ya biashara. Mazungumzo hayo yalisisitiza ushirikiano wa pamoja katika kuendeleza urithi wa kitamaduni na kupanua ushirikiano katika sekta ya habari na mawasiliano.




