TSN kuiunganisha serikali, wananchi

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) imetakiwa kuhakikisha inaisemea serikali kwa kila inachofanya ili kuimarisha mahusiano mazuri kati ya serikali na wananchi wake.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ametoa agizo hilo leo Machi 6, 2025, wakati wa ziara yake katika kampuni hiyo, iliyokuwa na lengo la kujitambulisha na kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchapisha magazeti kinachoendelea makao makuu ya kampuni hiyo Tazara, Dar es Salaam.

“Kama mnavyojua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, ninyi ni sehemu muhimu sana ya serikali hii, na tunategemea muwe mdomo wa serikali. Kwa hivyo, ni jukumu letu kuhakikisha huu mdomo unafunguka, na tutafanya hivyo kwa nguvu na maarifa yote ambayo Mungu ametupa,” amesema Mwinjuma.

Aidha, Mwinjuma ameihakikishia TSN kuwa serikali itajitahidi changamoto zinazokabili kampuni ili kuweka wafanyakazi katika mazingira mazuri ya kazi. Pia ameisisitiza TSN kuhakikisha inafanya kazi kwa bidii kuitetea serikali.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha uchapaji, Mwinjuma amesema: “Baada ya kutembelea mradi huu, naamini utakapokamilika, mapaka sasa upo kwenye asilimia 53.1, hivyo TSN itakuwa taasisi ya kipekee. Itaweza kujiendesha kwa ufanisi na pia kutoa huduma za uchapaji kwa taasisi nyingine zinazohitaji. Kwa sasa, tunafahamu kuwa TSN inachapisha magazeti yake mawili kupitia taasisi binafsi, jambo ambalo tunataka lifike mwisho. Kwa juhudi zilizowekwa na serikali, tunaamini hilo litawezekana.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi, amesema kuwa dira ya kampuni hiyo ni kuwa chombo cha habari cha kuaminika. Aidha, ameongeza kuwa moja ya majukumu yake ni kuwa daraja kati ya serikali na wananchi, jambo ambalo TSN imeendelea kutekeleza kwa weledi.
TSN ni kampuni inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLEO, Sunday News, SpotiLEO na habari za mitandaoni kupitia kitengo cha Daily News Digital.




