WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Mkundi Maalum inatarajia kuunda tume ambayo itazifuatilia taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati kuona endapo zimefungua madawati ya Jinsia ukiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali.
Naibu waziri wa wizara hiyo ,Mwanaidi Ali Khamis alisema hayo Februari 10, 2023 mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya namna bora ya uanzishaji na uendelezaji wa madawati ya jinsia katika vyuo kwa wakuu wa vyuo na waratibu wa madawati hayo kwa vyuo kutoka mikoa ya Tanga , Pwani na Morogoro.
Tume hiyo itafuatilia utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa Novemba 25, 2021 Jijini Dar es Salaam alipozindua kampeni ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuelekeza vyuo vyote nchini kuanzisha madawati ya kijinsia kwa ajili ya kutokomeza aina zote za ukatili maeneo ya vyuo .
Naibu Waziri alisema serikali kwa kushirikiana na wadau inemuwa ikitekeleza mpango kazi wa Taifa wa kutkomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ( MTAKUWWA) wa mwaka 2017/2018 – 2021/2022 ambapo muda wake umeisha Juni , 2022.
Mbali na hayo alisema mpango wa Mtakuwwa awamu ya pili wa mwaka 2023/2024- 2027/ 2028 unatarajia kuanza kutekelezwa muda sio mrefu na serikali imechukua jitihada mbalimbali za kukabiliana na vitendio vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Naibu Waziri alisema miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kuanzishwa madawati ya kijinsia katika taasisi ya elimu ya juu na elimu ya kati hapa nchini
“ Dawati hili litakuwa ni nyenzo muhimu ya kuweka ulinzi na mfumo wa kushughulikia matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo ikiwemo rushwa ya ngono kwani vitendo hivi havikubaliki kwa kuwa madhara yake ni makubwa “ alisema Mwanaidi
Naibu Waziri aliyataka taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati ambayo tayari yameazishwa madawati hayo kuhakikisha yanafuatilia kwa ukaribu vishiria na vitendo vya ukatili na kuchukua hatua stahiki.
Pia aliagiza madawati ya jinsia yanayofunguliwa katika vyuo yatumike kikamilifu kutoa elimu itakayowasaidia wanafunzi kujiamini katika maisha yao bila kupata bughudha na hofu ili waweze patikana viongozi bora watakao kuja kuiongoza nchi yetu.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) , Profesa Mussa Assad , alisema wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza wanapoingia vyuoni huwa hawajitambu vizuri “ulimbukeni” hususani wakike na wanaingia kwenye majaribu mengi kutoka kwa vijana wa kiume vyuoni na wengine wa mitaani .
Mimi kwa uzoefu wangu wa miaka miwili hapa Morogoro ni muhimu sana kuanzisha madawati ya jinsia kwenye vyuo ili kuwapa uelewa watoto wetu kuelezea maadili ya walimu na katika hilo ndani ya MUM halina nafasi kwa mwalimu anayehisiwa na taarifa za uhakika zinapopatikana kushiriki vitendo viovu anaondolewa mara moja “ alisema Profesa Assad
Naye Mkuu wa Chuo cha Polisi Kidatu, Kamisha Msaidizi wa Polisi , Zarau Mpangule alisema mmomonyoko wa maadili katika jamii ni chanzo kikubwa cha kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na vinachangiwa na kuunga utamaduni wa kimagharibi .
Mpangule alisema ili kupunguza ama kutomomeza vitendo hivyo ni vyema elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii iwe ni endelevu na katika kiwango kikubwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia , Rennie Gondwe alisema mafunzo hayo yaliwashirikisha washiriki 115 wakiwemo wakuu wa vyuo na waratibu wa madawati ya jinsia wa mikoa Tanga , Pwani na Morogoro ambayo ni mwendelezo kwa nchi mzima na yalianza katika mkoa wa Dar es Salaam.