MAOFISA kutoka Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wamefika kijiji cha Mganza wilayani Chato kuchunguza kifo cha Enos Misalaba (34) mtuhumiwa anayedaiwa kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime amesema hayo jana katika taarifa kwa waandishi na kueleza timu inaongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Misime alisema timu itafanya uchunguzi na kupata majibu ya taharuki iliyojitokeza na kupelekea ndugu kugoma kuzika mwili wa marehemu na wananchi kwenda kuchoma kituo cha polisi cha Kata Mganza wakidai polisi wamehusika.
“Timu ya kwanza imefanya kazi yake, wamekamilisha vizuri, wamekuja timu ambayo wanajua namna ya kufanya hiyo kazi, na nafikiri wataikamilisha wakati wowote, timu ya pili ndio ambao wametumwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi,”alisema.
Misime alisema mbali na uchunguzi unaoendelea lakini ni lazima wananchi wa Mganza na Chato kwa ujumla waacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani kosa haliwezi kutatuliwa kwa kufanya kosa lingine.
Aliwataka wazazi na walezi kuwafunda watoto kuacha vitendo vya uhalifu vikiwemo vya kujichukulia sheria mkononi kwa mihemuko kwa kuwa matokeo yake ni kifungo kinachowaumiza ndugu na jamaa.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mstaafu, Engelbert Kiondo aliwataka wakazi wa Mganza kuwafichua watu wanaoharibu amani na kuhatarisha usalama wa wengine.