WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amesema mwaka huu wanatarajia kukusanya Sh trilioni 1 kupitia sekta ya madini, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh bilioni 753 zilizokusanywa mwaka 2023/2024.
Mavunde ametoa taarifa hiyo leo Dar es Salaam aliposhiriki katika kikao kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini kujadili namba bora ya ushirikiano baina ya wizara hizi ili kukuza sekta ya madini.
SOMA: Wizara ya Madini waja kisasa zaidi
“Makusanyo ya mapato kupitia sekta ya madini yanaendelea kukua na kuongezeka kila mwaka mpaka kufikia Sh Bilioni 753 kwa mwaka 2023/24 na mwaka huu tumejipanga kukusanya Sh trilioni 1,” amesema Mavunde.
Akizungumza katika kikao hicho, kiongozi huyo amesema zipo changamoto kadhaa za kikodi ambazo Maml TRA wakikaa na wadau na kuzijadili kwa pamoja kutafuta suluhisho,sekta hii itapaa na kuwa mojawapo ya sekta kiongozi za kukuza uchumi wetu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya ameeleza umuhimu wa majadiliano na sekta ya madini kwa kuwa ni sekta ambayo mchango wake kwenye uchumi wa Tanzania unaonekana na hivyo kuelekeza TRA kukutana na wadau wake kwa haraka ili kupata ufumbuzi wa pamoja wa baadhi ya masuala ya kikodi yanayoleta changamoto.
Akitoa maelezo kwenye mkutano huo,Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda ameipongeza sekta ya madini kwa mchango wake mkubwa kwenye makusanyo ya kodi na kukuza uchumi wa Tanzania na kuahidi kuitisha kikao cha haraka ili kuzungumza na wadau juu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya madini ili kusaidia kuchochea ukuaji na mchango wa sekta katika uchumi wa Tanzania.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inajiandaa kufanya mkutano mkubwa na wadau wa sekta ya madini ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuiimarisha sekta ya madini na pia kuiongezea nchi mapato kupitia sekta hii.