‘Tumieni taarifa sahihi za hali ya hewa’

KATIKA kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuathiri maisha na uchumi, wananchi wametakiwa kuzingatia na kutumia taarifa sahihi za hali ya hewa ili kujikinga na majanga na kufanya maamuzi yenye tija katika shughuli zao za kila siku.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a, katika maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani Machi 23, 2026, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uangazi na matumizi ya data za hali ya hewa. SOMA: TMA yatoa tahadhari kwa wakulima,wafugaji
Amesema TMA itaendelea kuhimiza uwekezaji katika mifumo ya ufuatiliaji wa hali ya hewa ili kuwezesha utoaji wa tahadhari za mapema, hatua inayochangia kuokoa maisha, kulinda mali na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga ya hali mbaya ya hewa.

Chang’a ameeleza kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya kisasa ikiwemo rada za hali ya hewa, vituo vinavyojiendesha vyenyewe na mifumo ya kisasa ya uchakataji wa taarifa, hatua iliyoongeza usahihi wa utabiri na utoaji wa huduma kwa sekta mbalimbali kama kilimo, usafiri na nishati.
Kupitia ushirikiano na World Meteorological Organization (WMO) pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa kama Akili Mnemba (AI), TMA inaendelea kuimarisha huduma zake na kutoa mchango kimataifa, huku akisisitiza kuwa uwekezaji katika hali ya hewa ni msingi wa maendeleo endelevu na usalama wa taifa.



