Tumieni taarifa za sensa kuharakisha maendeleo – Majaliwa
MWANZA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wanaotekeleza afua mbalimbali za wanawake watumie taarifa na takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika kuandaa mipango na mikakati ya uwezeshaji wa wanawake nchini.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo ya Malkia wa Nguvu iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Kwa Tunza Beach jijini Mwanza, Majaliwa amewasisitiza wadau hao wanaotekeleza afua za wanawake waandae mipango yao kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali.
“Hii ni namna bora ya kuharakisha ustawi na maendeleo ya wanawake,” amesisitiza Mkuu huyo.
Soma pia: https://habarileo.co.tz/sensa-muhimu-katika-katika-kukuza-uchumi/
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuanzia Julai 2024 serikali itatoa utaratibu wa namna ya uendeshaji na utoaji wa mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Nitoe rai kwa wanawake wote na makundi ya vijana na watu wenye ulemavu wazingatie utaratibu utakaotolewa na niwakumbushe kuwa fedha inayotolewa ni mikopo siyo ufadhili hivyo wanufaika wote wawajibike kuirejesha,” amesema.
Amesema Serikali kwa mwaka 2023/2024 imetenga kiasi cha Sh bilioni 18.5 kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo kwa riba ya asilimia saba na kufanya makubaliano na NMB yatakayowezesha wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo wanawake kupata mikopo yenye riba nafuu.
Soma pia: https://youtu.be/t9fUrJbsdLE
“Ninafuraha sana kwa kuwa hamasa inayotokana na ushiriki wa Tuzo ya Malkia wa Nguvu imeendelea kuwavuta wanawake wengi zaidi na kuwafanya waongeze ubora wa shughuli wanazozifanya sambamba na kukuza biashara zao,” ameeleza kiongozi huyo.
Amesema anafahamu kuwa moja ya malengo ya Mradi wa Malkia wa Nguvu ni kuimarisha fursa za ajira na kuwa kichocheo muhimu cha uzalishaji wa ajira mpya. “Ninawapongeza sana kwa kuchangia jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.”