SONGWE; HALMASHAURI ya Mji Tunduma inategemea kukusanya kiasi cha Sh Millioni 80 mwaka wa fedha 2023/24 kupitia chanzo cha mapato cha maegesho ya magari makubwa kilichobuniwa a kumilikiwa na halmashauri hiyo kutokana na msongamano wa magari makubwa yaendayo nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Philmon Magesa alipofanya mazungumzoa na HabariLEO, akieleza kuwa kutokana na msongamano wa magari makubwa walitumia fursa hiyo kubuni mradi wa kituo cha maegesho, ambao magari hayo hulipia na kuwaingizia mapato ya ndani.
“Mji wetu wa Tunduma una msongamano mkubwa wa magari hasa magari makubwa ya mizigo kutoka nchi za SADC, hii ni kwa sababu Tunduma ni lango kuu unapoingia na unapotoka kuelekea nchi hizo.
“Sisi tumetumia msongamano kama fursa ya kutuongezea ukusanyaji wa mapato, tumebuni mradi wa kituo cha maegesho ya magari, ili madereva wanapokumbana na msongamano huo wapaki magari yao sehemu nzuri na rafiki.
“Pia parking hizi zipo za watu binafsi, lakini sisi kama halmashauri pia tuna parking yetu pia inayotusaidia kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri,’’ amesema Magesa.
Amesema mwaka wa fedha uliopita halmashauri ilitarajia kupata zaidi ya Sh milioni 60 kutokana na maegesho hayo, lakini mpaka mwaka wa fedha unaisha halmashauri ikawa imekusanya Sh millioni 70 kwa chanzo hicho kimoja cha maegesho ya malori, hivyo kudai mwaka huu wanatarajia kupata zaidi ya Sh milioni 80 kupitia chanzo hicho.
“ Chanzo hiki kimekuwa chachu ya halmashauri kuendelea kukusanya mapato mengi, fedha ambazo zimekuwa zikikusanywa zinatumika kuboresha huduma zingine za kijamii, kwa hiyo kinachofanyika ni kuzunguka kwa fedha kutoka mradi mmoja kwenda mradi mwingine lengo likiwa ni kuendelea kuikuza halmashauri yetu kwa mapato ya ndani na fedha kutoka serikali kuu, ” ameeleza.
Alisema maegesho hayo yana ubora zaidi kutokana na kuongeza ubunifu kwa kuongeza huduma zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba ya kulala wageni na sehemu ya kupata chakula.
Dereva wa gari la kubebea mizigo kwenda Zambia, Susanye Kinye alisema wanapenda kuegesha magari yao katika maegesho hayo kwa kuwa gharama yake ni nafuu, pia wanapendezwa na huduma mbalimbali zinazopatikana na pia ulinzi ni wa uhakika.