NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya Dk Grace Magembe amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Mara na Simiyu kuyatunza magari wanayokabidhiwa ili yaendelee kuwahudumia wananchi katika eneo la afya kwa muda mrefu zaidi.
Dk Grace amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kukabidhi magari manne kwa Makatibu Tawala waliowakilishwa na Waganga Wakuu wa Mikoa hiyo yaliyotolewa na Taasisi ya Amref Health Africa kwa ajili ya usimamizi shirikishi wa shughuli za Afya katika Mikoa hiyo.
“Magari haya yanapokabidhiwa kwetu tunaowajibu wa kuendelea kuyatunza na kuhakikisha yataendelea kufanya kazi vizuri ili kuhudumia wananchi,” Dk Grace.
Aidha Dk Grace ameendelea kupongeza ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Wadau mbalimbali wakiwemo Amref Health Africa kwa namna wamekuwa wakisaidia katika kutoa huduma mbalimbali za Afya kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Amref Health Africa hapa nchini Dk Frolence Temu amesema magari yaliyotolewa na Taasisi hiyo ni sita ambapo mawili yalitolewa awali katika Mkoa wa Simiyu na manne yametokewa jijini Dodoma ambapo matatu yataenda Mkoa wa Mara, moja Mkoa wa Simiyu na kufanya jumla ya magari matatu kwa kila Mkoa.