BENKI ya Selcom Microfinance Tanzania Limited imezindua rasmi huduma yake mpya ya kifedha ya kidigitali ijulikanayo kama SELCOM PESA, inayolenga kuleta mapinduzi katika sekta ya kifedha nchini kwa kutoa huduma rahisi, salama na nafuu kwa Watanzania wote.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba aliipongeza Selcom Microfinance kwa hatua hiyo, akisisitiza kuwa SELCOM PESA ni nyenzo muhimu katika kuongeza ushirikishwaji wa kifedha na kupunguza changamoto za gharama kubwa za miamala.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika ushirikishwaji wa kifedha, lakini bado changamoto za gharama za miamala na upatikanaji wa huduma bora za kifedha zinapaswa kushughulikiwa. SELCOM PESA inalenga kupunguza changamoto hizi kwa kutoa suluhisho la kifedha la gharama nafuu na linalopatikana kwa urahisi,” alisema Gavana Tutuba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Selcom Bank, Mheshimiwa Leonard Mususa, alieleza kuwa huduma hiyo imeunganishwa na Mfumo wa Malipo ya Haraka wa Tanzania (TIPS), ili kuwezesha miamala ya kifedha kufanyika kwa haraka na gharama nafuu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Selcom Bank, Leonard Mususa
“Uwekezaji huu wa kiteknolojia ni uthibitisho kuwa sekta binafsi inaweza kushirikiana na mifumo rasmi ya kifedha ili kuwapatia wananchi huduma bora kwa bei nafuu. SELCOM PESA inatoa huduma za kifedha zilizo salama, rahisi na zinazofikika kwa wote,” alisema Mususa.
Huduma ya SELCOM PESA inapatikana kwa kupakua programu yake kupitia Google Play au App Store, ambapo watumiaji wataweza kufanya miamala kama vile uhamishaji wa fedha kati ya benki na mitandao ya simu, malipo ya bili, na Malipo ya Serikali kupitia GePG.
Katika hafla hiyo, Selcom pia ilizindua kampeni yake mpya ya masoko ijulikanayo kama “5 kwa Jero”, inayolenga kuwapa wateja wake fursa ya kufanya miamala mitano kwa siku kwa gharama ya Tsh 500 tu.
Akielezea kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom Microfinance Tanzania, Julius Ruwaichi, alisema kuwa kampeni hiyo ni ya kipekee na inaleta mapinduzi makubwa kwa kuwawezesha wananchi kutumia huduma za kifedha bila mzigo wa gharama kubwa.
“Hii ni mara ya kwanza nchini Tanzania ambapo wateja wanapewa kifurushi cha kufanya miamala kwa ada maalum ya Tsh 500 tu kwa siku. Tunataka huduma za kifedha ziwe rafiki kwa kila Mtanzania,” alifafanua Ruwaichi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom Microfinance Tanzania, Julius Ruwaichi
Uzinduzi wa SELCOM PESA unaendelea kuonyesha juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhimiza matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya kiuchumi na kifedha nchini. Gavana Tutuba alihitimisha kwa kupongeza Selcom Microfinance Tanzania na mshirika wake Selcom Paytech Limited kwa hatua hiyo ya maendeleo, akisisitiza kuwa huduma hiyo inatarajiwa kuleta mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini.
Hi there, just wanted to say, I enjoyed this blog post.
It was helpful. Keep on posting!