RAIS Samia Suluhu Hassan amemteua Emmanuel Tutuba kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Awali Tutuba alikua Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 7, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, imesema Tutuba amechukua nafasi ya Profesa Florens Luoga ambae amemaliza muda wake.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba Rais Samia amemteua pia Dk Natu Mwamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango akichukua nafasi ya Tutuba.
“Dk Mwamba alikuwa mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya uendeshaji wa kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (Kadco),” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya Ikulu inaeleza kwamba uteuzi huo unaanza mara moja.

Profesa Luoga aliteuliwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, Oktoba 23, 2017 akichukua nafasi ya Benno Ndulu ambaye alistaafu kama Gavana wa BOT
Profesa Luoga, ameiongoza BOT kwa miaka mitano.