Ushiriki ‘Samia Kalamu Awards’ wasogezwa mbele

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameutaarifu umma kuwa tuzo za waandishi wa habari za maendeleo walizoita ‘Samia Kalamu Awards’ muda wa kuomba kushiriki katika tuzo umesogezwa mbele hadi Oktoba 30, 2024.

Tuzo hizo zenye kauli mbiu ya ‘Uzalendo ndio Ujanja’ zikiwa na lengo la kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira ya nchi ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa kutangaza tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa (TAMWA) Dk Rose Reuben amesema tuzo hizo zitahusisha maudhui yaliyochapishwa kupitia magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni akisisitiza kuwa ni tuzo maalumu kwa vyombo vya habari na maofisa habari wa serikali.

Advertisement

“Tunapenda kuwa taarifa waandishi wa habari kuwa tuzo hizo zimepelekea mbele hadi Oktoba 30, 2024 kuwapa nafasi waandishi waliokutana na changamoto ya kiufundi katika wakati wa kupandisha kazi zao,”

“Tuzo hizo zitatolewa kwa waandishi wa habari wa Kitanzania ili kuhamasisha kukuza na kupanua wigo wa uandishi, utangazaji na uchapishaji wa mahudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari asili na mitandao,” amesema.

Amesema matarajio ni kwamba Samia Kalamu Awards zitahamasisha uandishi wa habari unaozingatia weledi, maadili, kukuza maendeleo ya Tanzania na uzalendo hivyo amemhamasisha kila mwanahabari kutumia fursa hiyo kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti ya https://samiaawards.tz

“Kutokana na maendeleo ya teknolojia na utandawazi, uandishi wa habari nchini umekuwa ukijikita kwenye kuburudisha, kuhabarisha huku uandishi wa makala za kuelimisha zikiwa kwa kiwango kidogo lakini pia vyombo vya habari nchini vimekuwa vikitangaza maudhui ya nje yasiyokidhi mahitaji ya hadhira ya Kitanzania.

Na kwa muktadha huo, TAMWA kwa kushirikiana na TCRA tuliamua kutoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari, watangazaji , wahariri, mameneja, maofisa habari, wamiliki wa vyombo vya habari, wahadhiri na watengeneza maudhui wa mitandaoni wapatao 2,054 kote nchini kwa kipindi cha miezi mitatu mwaka huu 2024”,ameongeza Dk Rose.

Amefafanua kuwa, pamoja na mafunzo hayo wameona ni vyema kutoa tuzo kwa wanahabari pamoja na vyombo vya habari ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kuandika, kuchapisha na kutangaza maudhui ya ndani hasa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi wenye tija kwa watanzania.

“Tuzo hizi zimepewa jina la Samia Kalamu Awards ili kutambua na kuenzi historia ya kuwa na Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na zinatarajiwa kutolewa Novemba 2024 zikiwa katika makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalum za kitaifa, Tuzo kwa vyombo vya habari na Tuzo za Kisekta”,amesema Dk Rose.

Amevitaja vigezo vya ushiriki kuwa ni makala zinazoshindanishwa ziwe zinahusu masuala ya maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi na fursa zinazopatikana kutoka kwenye miradi mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabir Bakari amesema kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na hazijawai kuwasilishwa kuwaniwa tuzo zingine.

“Kazi zote zinatakiwa kufata taratibu za haki milikiwaandishi wanatakiwa kuwasilishwa kazi zao kupitia tovuti rasmi ya tuzo www.samiaaward.tz taarifa za kushiriki zinapatikana kwenye tovuti.

Ameongeza kuwa zoezi la upigaji kura litaanza Novemba 8, 2024 ili kuchagua kazi bora zitakazokuwa zimewasilishwa.