Twiga safi Wafcon

TWIGA Stars imefuzu hatua ya pili ya kufuzu Mataifa ya Afrika (WAFCON 2026) licha ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Equatorial Guinea, Uwanja wa Cano Sports Academy jijini Malabo nchini Equatorial Guinea jana.
Faida ya ushindi wa mabao 3-1 waliyopata Twiga Stars nyumbani imewasaidia kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya kufungana bao 1-1.
Kwa ushindi huo Twiga Stars itacheza na Ethiopia ambao wameitoa Uganda kwa penalti 5-4 baada ya kumaliza mchezo kwa sare ya 2-2, mchezo wa kwanza Uganda walishinda 2-0 na jana Ethiopia wakashinda 2-0 wakalazimika kupiganiana penalti kupata mshindi.
Katika mchezo wa jana Twiga Stars walisawazisha bao dakika ya 71 lililofungwa na Enekia Kasonga akisawazisha bao la mapema la dakika 12.
Katika mchezo huo Twiga Stars iliwakosa washambuliaji, Clara Luvanga na kiungo, Joyce Lema ambao ni majeruhi baada ya kuumia kwenye mchezo wa awali na hawakusafiri na timu.
Twiga Stars ikifuzu fainali hizo, itaungana na timu nyingine za taifa za Tanzania zilizofuzu kwenye mashindano makubwa ya Afrika, Taifa Stars iliyofuzu Afcon, Serengeti Boys iliyofuzu Afcon U17 na Ngorongoro Heroes iliyofuzu Afcon U20.
Twiga Stars ipo nafasi ya 145 katika viwango vya ubora wa soka la wanawake duniani, pia ni miongoni mwa timu 12 zilizofuzu Wafcon 2024 itakayofanyika mwaka huu Morocco kuanzia Julai 5 hadi 26.



