Ubongo yatangaza msimu mpya wa elimu kwa watoto

DAR-ES-SALAAM : SHIRIKA la Ubongo limetangaza rasmi uzinduzi wa msimu wa tano wa kipindi maarufu cha watoto, Akili and Me, ukiwa na muonekano mpya, teknolojia ya kisasa ya uhuishaji, na msisitizo maalum katika maendeleo ya kijamii na kihisia kwa watoto wadogo.
Ubongo, ambalo linatambulika kama Shirika kinara Barani Afrika katika kuunganisha elimu na burudani, limefanikiwa kuwafikia zaidi ya watoto milioni 48 kupitia vipindi vyake vya Akili and Me na Ubongo Kids.
Msimu huu mpya umejikita katika mafunzo ya kijamii na kihisia (SEL), yakilenga kuwasaidia watoto kutambua, kuelewa, na kueleza hisia zao kwa njia chanya.
“Kupitia msimu huu, tulitaka kwenda zaidi ya ABC na 123 kwa kuangazia kitu cha msingi zaidi—kuwasaidia watoto kuelewa na kueleza hisia zao,” amesema Tamala Maerere-Kateka, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano ya Kimkakati wa Ubongo.
Ameongeza kuwa watoto wanapojifunza kushughulikia hisia zao, hujenga ujasiri na ustahimilivu unaohitajika kufanikiwa shuleni na katika maisha ya kila siku.
Kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, wahusika wa kipindi wamebuniwa upya kwa rangi na
sura zenye mvuto zaidi kwa watoto. SOMA: Vipindi vya Ubongo vyafikia familia mil 32
Ubongo pia imezindua Akili and Me Games kupitia programu ya Ubongo Playroom ambayo inajumuisha video za elimu, vitabu, hadithi za sauti, na michezo ya kielimu kwa ajili ya kuongeza ushiriki wa watoto katika kujifunza kwa njia ya kucheza. Kwa taarifa zaidi kuhusu msimu huo mpya, tembelea: www.akiliandme.com