Uchukuzi, Elimu, Maji kuwasilisha bajeti wiki hii

DODOMA; WIZARA ya Uchukuzi leo inatarajiwa kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Wiki hii bajeti ya Wizara ya Uchukuzi itafuatiwa na ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wabunge watahitimisha kwa kujadili makadiro ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji.

Kwenye bajeti ya Wizara ya Uchukuzi mambo yanayotarajiwa kujitokeza ni utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR), sekta ya usafirishaji katika sekta ya anga, bandari na reli.

Advertisement

Kwa makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hoja za utekelezaji wa sera na mitaala mipya na mikopo ya elimu ya juu na kati na ufadhili kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi zinatarajiwa kujitokeza.

Aidha, wabunge pia watakuwa na kazi ya kujadili makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Maji ambapo hoja kubwa inayotarajiwa kujadiliwa ni hali ya upatikanaji wa huduma za maji mijini na vijijini. Mpaka sasa Bunge limepitisha mapato na matumizi kwa mwaka 2024/24 kwa wizara tisa.

Wizara hizo ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira.

Pia Bunge limepitisha mapato na matumizi kwa Wizara ya Nishati, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Madini na Wizara ya Kilimo