‘Uchumi umeimarika, mfumuko wa bei umepungua’

DAR ES SALAAM; Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali .

Maboresho hayo yana lengo la kukuza uchumi unaotarajiwa kuimarika kwa siku zijazo kutokana jitihada za uboreshaji wa miundombinu hususani reli, barabara na bandari, upatikanaji wa uhakika wa umeme, hali nzuri ya hewa kwa shughuli za kilimo pamoja na sera za programu za maboresho.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu (BoT,) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha Dk Yamungu Kayandabila, wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC,) ya Bodi ya Wakurugenzi wa BoT  iliyoketi Julai 3, 2024.

Amesema katika kutathimini mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati hiyo ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza ya mwaka na pili ya mwaka 2024.

” Mfumuko wa bei umeendelea kupungua pamoja na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani na benki kuu katika nchi nyingi kuanza kupunguza viwango vya riba….Bei ya mafuta ghafi ilipungua licha ya kuongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi Juni 2024,

“Bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama njia mbadala ya uwekezaji katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani, na matarajio ni uchumi wa dunia kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024 na 2025 licha ya kuwepo kwa hatari kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mizozo ya kibiashara,”  ameeleza.

Pia amesema, tathmini iliyofanywa na kamati hiyo kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba, utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2024 umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia 5.

” Uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara, mwaka 2023 ulikua kwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2022 na mwenendo huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, chakula na uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi na mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na 2025,” amefafanua

Amesema mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu na chini ya lengo la Taifa la chini ya asilimia 5, Mwezi Aprili na Mei 2024 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3 na 3.1 mwenendo uliosababishwa na kupungua kwa mfumuko wa bei ya chakula kufuatia uwepo wa chakula cha kutosha nchini na kwa upande wa Zanzibar mfumuko wa bei umeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 5 kutokana na kupungua kwa bei za chakula na bidhaa zisizo za chakula na mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki ndani ya wigo wa asilimia tatu hadi nne katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na kuendelea.

Dk Yamungu amesema, utekelezaji bajeti ya Serikali umeendelea kuwa wa kuridhisha huku ukichagiza utekelezaji sera ya fedha ambapo; mapato ya Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia asilimia 95 ya lengo na Zanzibar mapato yakivuka lengo kwa asilimia 0.3 kulikosababishwa na maboresho katika usimamizi wa kulipa kodi na kuongezeka kwa utayari wa wananchi kulipa kodi.

Akifafanua kuhusu akiba ya fedha za kigeni, amesema akiba iliendelea kuwa ya kutosha ya zaidi ya dola bilioni 5 zinazotosheleza uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa zaidi ya miezi minne, huku matarajio yakiwa ni kuongezeka zaidi kwa fedha za kigeni nchini kupitia mapato yatokanayo na shughuli za utalii, mauzo ya madini, bidhaa asilia na usafirishaji wa chakula kwenda Nchi jirani.

Habari Zifananazo

Back to top button