UNHRC kuujadili mgogoro wa Congo

GENEVA: KHOFU yaongezeka juu ya uwezekano wa waasi wa M23 kusonga mbele kuuchukuwa mji wa Bukavu,Kivu Kusini.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linajiandaa kufanya kikao cha dharura siku ya Ijumaa, kuujadili mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Msemaji wa baraza hilo Paschal Sim amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba kikao hicho kimeitishwa kufuatia ombi la serikali ya Congo lililotolewa Jumatatu.
Baraza hilo kimsingi ndio chombo cha juu zaidi katika Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya haki za binadamu na kwa hakika kilikuwa hakina ratiba ya kukutana hadi mwishoni mwa Februari.
Waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda wiki iliyopita waliuteka mji wa Goma huko Kivu Kaskazini eneo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa Kongo na kusababisha umwagaji damu kwenye eneo hilo.


