Uingereza yafuta ushuru bidhaa za Tanzania

SERIKALI ya Uingereza imefungua milango kwa bidhaa za Tanzania kulifikia soko la nchi hiyo bila kutozwa ushuru.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara anayehusika na Uwekezaji, Ally Gugu, Balozi wa Uingereza nchini, David Concar na Mwakilishi Maalumu wa masuala ya biashara wa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa Tanzania, Lord Walney walisema hayo Dar es Salaam jana.

Waliwaeleza waandishi wa habari kuwa Serikali ya Uingereza kupitia ubalozi wake nchini kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, zilifanya kongamano lao la pili la mwaka la biashara jijini Dar es Salaam jana.

Gugu alisema Uingereza ni moja ya wawekezaji wakubwa wanaofanya biashara na kuwekeza nchini na mara nyingi hushika ama nafasi ya kwanza ya pili kwa uwekezaji nchini.

Alisema ili kuimarisha ushirikiano huo wa kibiashara na uwekezaji, Tanzania na Uingereza ziliona kuna haja ya kuanzisha kongamano hilo ili kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, masuala ya kisera na changamoto wanazokutana nazo.

Alisema maoni na mapendekezo yatakayopatikana yataiwezesha serikali kuona namna kuboresha sera, sheria na taratibu zake ili kuvutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara hususani kutoka Uingereza.

“Mwaka jana tulikuwa na kampuni takribani 13 zilizoshiriki moja kwa moja kwenye mkutano na wengine walishiriki kwa njia ya mtandao. Katika mkutano huu, tuna wageni wasiopungua 30 kutoka Uingereza zikiwemo kampuni, viongozi wa kampuni na taasisi za umma upande wa Uingereza,” alisema Gugu.

Aliongeza “Tutakuwa na majadiliano kati ya taasisi za umma za Tanzania na za Uingereza, pia kutakuwa na majadiliano kati ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na Uingereza na kisha tutakuja pamoja kukubaliana mambo ya msingi na kuweka mikakati ya kufuatilia utekelezaji wake.”

Kwa mujibu wake, moja ya manufaa yaliyopatikana katika kongamano la kwanza mwaka jana ni kuja kwa kampuni kadhaa za Uingereza ambazo zilikutanishwa na sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini, utalii na nyinginezo kwa upande wa Bara na Zanzibar.

Pia alisema serikali itatoa taaarifa ya utekelezaji wa maboresho kibiashara na mazingira kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini ili kuwapa hamasa Waingereza kuona kuwa Tanzania iko tayari kuwakaribisha na kufanya nao biashara.

Balozi Concar alisema Uingereza imeandaa mpango maalumu wa kuziwezesha nchi zinazoendelea za Afrika ikiwamo Tanzania kufaidika na soko lao.

Alisema kupitia mpango huo, asilimia 99 ya bidhaa za Tanzania zinazozalishwa nchini zitanufaika kwa kulifikia soko la Uingereza bila kutozwa ushuru ili ziwe shindani.

“Ili bidhaa ipewe upendeleo wa kutotozwa kodi, vigezo vya uasili wa bidhaa utazingatiwa kwa maana kwamba bidhaa lazima iwe imezalishwa Tanzania, tutaweka vigezo rafiki na rahisi ili bidhaa za Tanzania zifike katika soko la Uingeereza,” alisema Balozi Concar.

Mwakilishi Maalumu wa Masuala ya Biashara wa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa Tanzania, Walney, pamoja na mambo mengine, alisema ameleta kundi la wafanyabiashara zaidi ya 20 ili kuimarisha biashara na uwekezaji na kuleta ustawi wa nchi zote mbili.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kusaidia wawekezaji na wafanyabiashara, natazamia kufanya kazi na Serikali ya Tanzania na sekta binafsi na kuweka mazingira mazuri kwa biashara za Uingereza na Tanzania kustawi,” alisema Walney.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x