Ujerumani yaahidi dola milioni 680 kusaidia Ukraine

UKRAINE: KANSELA wa Ujerumani Olaf Scholz amefanya ziara ya kushtukiza nchini Ukraine ili kuthibitisha uungaji mkono wa Berlin kwa Kyiv katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Akizungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky  amesema serikali yake itaendelea kuisaidia Ukraine kwa kuendelea kutoa msaada wa kijeshi  wenye thamani ya dola milioni 680 utakaowasilishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Ziara ya Scholz inafanyika huku vikosi vya Ukraine vikipata pigo katika mstari wa mbele wa vita kutokana na mashambulizi makubwa ya Moscow ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya nishati ikiwemo gridi ya taifa ya umeme.

Advertisement

Sholz anazuru Ukraine wakati taarifa zikisema, wanajeshi wa Ukraine walioko mstari wa mbele wameelemewa na vita.

Wakatihuohuo, Urusi bado inaendelea kushambulia miundombinu ya nishati na kuongeza hofu kubwa kwa watu wa nchi hiyo ambayo kwa sasa inaingia  kwenye kipindi cha baridi.

Lakini pia wasiwasi wa Marekani kuondoa msaada wa kijeshi kwa taifa hilo mara baada ya Rais mteule Donald Trump kuingia madarakani mwezi Januari mwakani, nacho ni kitisho kingine kinachoweza kuongeza ugumu zaidi kwa upande wa Ukraine inayopigana na Urusi kwa zaidi ya siku 1,000 sasa.

SOMA: Ukraine: miili ya wanajeshi 563 yapokelewa