WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, ameishukuru Ujerumani kwa kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi yake ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vya ufundi (VETA) vitakavyosaidia kukabiliana na tatizo la ajira hususani kwa vijana nchini.
Nchemba aliyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, kutoka Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Dk Barbel Kofler, jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa kipaumbele cha serikali ni kujenga vyuo hivyo vya ufundi katika wilaya 72 ambazo hazina kabisa vyuo hivyo ili kutekeleza dira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutatua changamoto ya ajira inayowakabili wananchi wake na kuiomba Ujerumani kusaidia ujenzi wa miundombinu ya vyuo hivyo pamoja na zana za kufundishia na kujifunzia.
“Eneo ambalo tumelizungumzia linaenda sambamba na mwelekeo wa Rais Samia wa ujenzi wa vyuo vya ufundi (Veta) katika maeneo ya wilaya ambazo hazina vyuo vya ufundi ili kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira,” alisema Mwigulu.
Alimshukuru Dk Kofler kwa utayari wa serikali yake wa kusaidia utekelezaji wa miradi ya kiuchumi na kijamii ambayo nchi hiyo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za afya, elimu, hifadhi ya mazingira, utalii, afya na mingine mingi.
Kuhusu masuala mengine ya usawa wa kijinsia na udhibiti wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, waziri huyo, alimhakikishia Kofler kwamba Serikali imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na masuala hayo. Alisema kuwa uwakilishi wa wanawake katika vyombo ya maamuzi umeongezeka na hatua madhubuti zinachukuliwa kukabiliana na vitengo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, aliipongeza Ujerumani kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuwa hivi karibuni nchi hizo mbili zilitiliana saini mikataba mitatu yenye thamani ya Euro milioni 45 sawa na takribani Sh bilioni 119.2 ya kutekeleza miradi ya maji, afya na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.
Kwa upande wake, Kofler aliipongeza serikali kwa jitihada wanazozifanya za kukuza uchumi, kuimarisha demokrasia na kuimarisha afya ya jamii na kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.
Alisema kuwa nchi yake iko tayari kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vya ufundi ambavyo alisema ni muhimu katika maendeleo ya nchi na kwamba uwekezaji unaofanywa na mashirika na taasisi mbalimbali nchini unahitaji nguvu kazi yenye ujuzi.
Comments are closed.