Ujumbe wa Rais Samia kwa Kapteni Ibrahim wa Burkina Faso

OUAGADOUGOU – Mjumbe Maalum wa Rais Samia Suluhu Hassan, na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amehitimisha ziara yake nchini Burkina Faso kwa kukutana na Rais wa nchi hiyo, Kapteni Ibrahim Traoré.

Mkutano huo muhimu wa kidiplomasia umefanyika jijini Ouagadougou na kuhudhuriwa na maafisa waandamizi kutoka Serikali za Tanzania na Burkina Faso. Katika mazungumzo hayo, Dk. Kikwete alimkabidhi Rais Traoré ujumbe maalum kutoka kwa Rais Samia, akieleza kuwa ni heshima kubwa kuwasilisha ujumbe huo kwa niaba ya taifa.

“Rais wangu amenituma nije kuwasilisha Ujumbe Maalum kwako, na ninafurahi kwa kunipokea na kukubali rasmi ujumbe huu leo,” alisema Dk. Kikwete.

Mbali na kuwasilisha ujumbe, Dk. Kikwete aliwasilisha salamu za heri kutoka kwa Rais Samia, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya kidugu baina ya mataifa ya Afrika. Alisisitiza kwamba kwa kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutumia kwa pamoja maarifa ya kitaifa, bara la Afrika lina nafasi ya kutumia rasilimali zake kwa maendeleo ya wananchi wake.

Mkutano huu unakuja katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na nchi mbalimbali za Afrika, ikiwa ni sehemu ya sera ya kidiplomasia ya kiuchumi na ushirikiano wa kusini kwa kusini (South-South Cooperation).

 

Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traoré akisalimiana na Mjumbe Maalum wa Rais Samia Suluhu Hassan, na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traoré akipokea Ujumbe Maalum wa Rais Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa Rais Mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

 

Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traoré akisalimiana na Profesa Mohamed Yakub Janabi, Mshauri wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Masuala ya Afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mgombea wa kiti cha Ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani – Afrika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button