LONDON, UINGEREZA – Kupima mate kunaweza kuwa njia mpya ya kubadili mkondo wa mapambano dhidi ya saratani ya tezi dume, kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na wanasayansi nchini Uingereza.
Katika utafiti huo, wataalamu wamebaini kuwa kuchambua sampuli ya mate kwa ajili ya kuchunguza vinasaba (DNA) vya wanaume kunaweza kusaidia kubaini wale walio katika hatari kubwa ya kuugua saratani hiyo. Mbinu hiyo ilitumika pamoja na uchunguzi wa MRI na kipimo cha PSA, na kufanikisha kugundua baadhi ya aina hatari za saratani ambazo huchukua muda mrefu kutoa dalili.
Pamoja na matumaini hayo, wataalamu wanasema bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa njia hiyo mpya inaokoa maisha. Aidha, inakadiriwa kuwa huenda ikachukua miaka kadhaa kabla ya teknolojia hiyo kuanza kutumika katika huduma za kawaida za afya.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wanaume 12,000 hufariki kila mwaka kutokana na saratani ya tezi dume nchini Uingereza. Wito wa upimaji wa mapema umeongezeka kufuatia tangazo la mwanariadha wa Olimpiki, Sir Chris Hoy, kuhusu kupatwa na saratani ya hatua ya mwisho ya tezi hiyo.
Profesa Dusko Ilic wa Chuo Kikuu cha King’s College London amesema kuwa ingawa vipimo hivyo vinaongeza uwezo wa kugundua saratani, bado kuna haja ya kufanya tafiti zaidi ili kuthibitisha kama vinaongeza muda wa kuishi au kuboresha maisha ya wagonjwa.
Kwa sasa, utafiti huo unawajumuisha watu wa asili ya Ulaya pekee, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha unajumuisha pia watu kutoka jamii nyingine, hasa wa asili ya Kiafrika ambao wapo kwenye hatari mara mbili zaidi ya kuugua saratani ya tezi dume.
Jaribio hilo la mate limeingizwa katika utafiti mkubwa wa Transform, unaolenga kutafuta njia bora ya kuanzisha mpango wa kitaifa wa upimaji wa saratani ya tezi dume.
SOMA: Daktari ahimiza kupima tezi dume
There’s definately a lot to learn about this issue.
I like all of the points you have made.