BODI ya Sukari nchini (SBT) imewataka Watanzania kudai risiti wanaponunua sukari kwa bei tofauti na iliyoelekezwa na wachukue hatua kisheria .
Imesema hatua hiyo ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika kwa kuwa tayari tani 6000 za sukari kutoka nje ya nchi zimeingia nchini na kuanza kupelekwa katika baadhi ya mikoa ili isambazwe na kuwafikia wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Profesa Keneth Bengesi amesema hayo Dar es Salaam na kuwataka wafanyabiashara kuwa waaminifu na kutokuwa na tamaa ya kutaka faida.
Kuhusu kuingia kwa sukari amesema ndani ya siku tatu kuanzia juzi kiwango hicho kimeshaingia na kuanza kupelekwa mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam,hatua itakayosababisha sukari kuuzwa kwa mujibu wa bei elekezi.
“Bei ya sukari inatakiwa kushuka haraka iwezekanavyo na iuzwe kwa mujibu wa bei elekezi, ni muhimu kila mnunuzi kuhakikisha anapatiwa risiti pindi anunuapo na kuchukua hatua za kutoa taarifa kwa mamlaka husika iwapo bei ni tofauti,” amesema Profesa Bengesi.
Almesema licha ya kiwango hicho cha sukari kuingia lakini hadi kufikia katikati ya Februari tani zaidi ya 30,000 zitaingizwa na pia bodi itaendelea kufanya mapitio kuona kama kuna haja ya kuongeza sukari zaidi ingawaje mipango ni uagizaji wa sukari unafanywa hadi kufikia Juni mwaka huu.
“Hakuna anayetakiwa kuuza sukari zaidi ya bei inayotakiwa, wapo watu ambao wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” ameonya Profesa Bengesi na kuahidi kuwa sukari iliyoingizwa itasambazwa kwenye maduka mengi.
Amesema hata sukari ya nje haitakiwi kuzidi bei elekezi kwa kuwa serikali imesamehe kodi ya ushuru wa forodha na hata VAT kwa waagizaji ambapo msamaha huo unakwenda hadi kwa walaji.
Kuhusu sababu za kupungua kwa sukari nchini, Profesa Bengesi amesema ilitokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo mafuriko ya maji yalijaa kwenye viwanda na hata kwenye mashamba ya miwa na kuvuruga uzalishaji.
Hata hivyo amesema iwapo tatizo hilo lisingetokea tayari uzalishaji ungefikia tani 560,000 kwa mwaka huku mahitaji yakiwa ni tani 552000.
“Uzalishaji wa sukari ungeongezeka kutokana na ukamilishaji wa viwanda vipya lakini pia upanuzi na uboreshwaji uliofanywa kwa viwanda vilivyopo,” amesema Profesa Bengesi na kutolea mfano kiwanda cha Kilombero ambacho kilipanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 130,000 kwa mwaka hadi tani 271,000.
“Hatujawahi kujitosheleza kwa sukari lakini juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali tangu nchi ilipopata Uhuru kukiwa na viwanda vinne tu na ambavyo vimekuwepo ndani ya miaka 50 ,” amesema.
Amesema kwa kipindi hicho viwanda vilikuwa vikitakiwa kuzalisha tani 230,000 kwa mwaka lakini kiuhalisia vikizalisha tani 110,000 huku mahitaji yakifikia tani 300,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 110,000 hiyo ikiwa ni mwaka 2001.
Profesa Bengesi amesema kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na matumizi kuongezeka sukari haijatosheleza.
Kuhusu jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali kuanzia mwaka 2017 ili kuepuka usumbufu kwenye bidhaa hiyo amesema ni pamoja na kuangalia mfumo wa uagizaji nje ya nchi kwamba wazalishaji wa ndani ndio waagize na pia kutengeneza mazingira ya uwekezaji ili viwanda vilivyokuwepo vifanye upanuzi mkubwa.
Amesema katika kipindi hicho viwanda vilipanua uzalishaji na kutoka tani 293000 hadi tani 460,000 huku kukiwepo jitihada za kuongeza viwanda vipya.
Amevitaja viwanda vilivyopo hadi sasa nchini kuwa ni pamoja na Kilombero, Mtibwa, TPC, Kagera, Bagamoyo, Mbigiri na Manyara huku vingine vipya vyaRufiji na Kasulu vikitarajiwa kukamilika na kuongeza wigo wa uzalishaji wa sukari nchini.