KWA mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) za mwaka 2022, sekta isiyo rasmi nchini Tanzania imekuwa nguzo kuu ya uchumi wa taifa.
Sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 50 ya Pato la Taifa huku pia ikitoa ajira kwa zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi wake.
Mtaalamu wa masuala ya fedha kutoka Ruislip, London Magharibi nchini Uingereza, Brianna Johnson anasema, “Sekta hii ina uwazi, ustahimilivu na uwezo wa asili wa kuondoa au kupunguza umaskini. Hata hivyo, bado kampuni
nyingi zisizo rasmi ziko nje ya mfumo rasmi wa kodi.”
Anasema hali hii ya kampuni nyingi kuwa nje ya mfumo wa kodi si lazima kwamba inatokana na ukwepaji kodi wa makusudi, bali inatokana zaidi na uwepo wa taratibu ngumu zenye urasimu, vikwazo vya kifedha na hofu kubwa ya
kutozwa faini ya kikodi.
Makala haya leo yanashughulikia changamoto hizi kwa kuwasilisha mkakati wa kina wa maboresho ya kodi unaotokana na uchanganuzi wa kitaalamu na vipimo thabiti.
Lengo kuu la makala haya ni kuipa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi maoni muhimu kutokana na mitazamo ya umma kuhusu ujumuishaji wa sekta isiyo rasmi ya nchini katika uchumi rasmi, na hatimaye kukuza zaidi mfumo jumuishi na endelevu wa kifedha.
Mazingira ya Kodi
Mtaalamu wa masuala ya kodi kutoka Algeria ambaye kwa sasa yuko likizo Karatu mkoani Arusha, Yasmine Yassine anasema mfumo wa kodi wa Tanzania hautabiriki na umepitwa na wakati mambo yanayofanya usifae kwa sekta isiyo rasmi.
Anasema wakati Sheria ya Fedha ya 2020 ililenga kurahisisha usajili wa kodi, athari zake zimekuwa ndogo kwani wafanyabiashara wengi wameachwa nje ya mfumo rasmi.
Tathmini hiyo inaungwa mkono na mshauri wa masuala ya fedha aliyeko Babati mkoani Manyara, Hussein Kilokoza anayenukuu ripoti za KPMG na PwC za 2020 zinazobainisha kuwa, licha ya kuwapo maboresho ya kodi hivi karibuni, biashara nyingi hazijasajiliwa.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti, Sheria ya Fedha haijaondoa vikwazo vya kimuundo vinavyokwamisha urasimishaji wa biashara zisizo rasmi. Matokeo hayo yanathibitisha zaidi hoja ya Yassine kuwa, mfumo wa ulipaji kodi uliopo Tanzania hauendani na hali halisi inayowakabili wafanyabiashara wadogo wanaofanya shughuli zao nje ya uchumi rasmi.
Kwa msingi huo, uchanganuzi wa takwimu zilizopo unaonesha kuwa, asilimia kati ya 20 hadi 30 pekee ya biashara
zisizo rasmi ndizo zimesajiliwa.
Utafiti kuhusu biashara isiyo rasmi uliofanywa na Benki ya Dunia mwaka 2023 ulibainisha biashara zisizo rasmi 2,433 katika maeneo kadhaa ya Dar es Salaam kwa kubaini ukubwa wa sekta hiyo. Kwa kuzingatiwa kuwa kwa
ujumla maeneo ya mijini yana viwango vya juu vya usajili kuliko vijijini, asilimia ya kitaifa inaweza kuwa chini.
Hii inaonesha kuwa, biashara milioni 3.5 hadi 4 zisizo rasmi hazijasajiliwa na hivyo kuwapo hitaji la maboresho ya
kodi yanayorahisisha usajili, ufikiaji wa fedha na maboresho yanayolenga kujenga imani. Urasimishaji unaweza kupanua wigo wa vyanzo vya kodi na kuzipa biashara usaidizi wa kifedha na motisha za serikali.
Mshauri wa masuala ya kodi anayeishi Dodoma, Brian Macha anasema watendaji wasio rasmi, wakiwemo wachuuzi wa mitaani (wamachinga) na madereva wa bodaboda huhama mara kwa mara na hivyo kuwa vigumu kwa mamlaka za kodi kufuatilia mapato na kutekeleza wa kanuni na sheria za kodi.
Kimsingi, mtindo au mfumo wa kodi uliopo umeshindwa kumudu mabadiliko ya mara kwa mara ya mtiririko wa
fedha katika sekta rasmi, hivyo kuzitenganisha zaidi biashara zisizo rasmi. Ni muhimu kuwapo mtazamo unaobadilika ili kukuza ushirikiano endelevu wa kiuchumi.
Vikwazo utekelezaji sheria za kodi
Kwa mujibu wa Brian Macha, kutegemea mzunguko wa fedha wa kila siku na ukosefu wa huduma za kifedha hufanya ulipaji kodi kuwa changamoto kwa wamiliki wa biashara zisizo rasmi. Hii ni kwa kuwa wafanyabiashara wengi huogopa wakidhani kuwa, urasimishaji biashara utawapa mizigo wa kodi isiotabirika na kuathiri faida kidogo wapatayo.
Aidha, kutoaminiwa kwa mamlaka za kodi kutokana unyanyasaji, kutoza kodi bila utaratibu na usimamizi usioeleweka hupunguza utekelezaji wa sheria za kodi. Taarifa zinaonesha kuna asilimia 25 ya wafanyabiashara wasio rasmi wa mijini katika nchi 5 za juu kiuchumi barani Afrika.
Nchi hizo ndizo zinazojenga asilimia 50 ya Pato la Taifa la Afrika la Dola za Marekani trilioni 2.4 wanakumbwa na
unyanyasaji unaohusiana na masuala ya kodi, hivyo kuweka vikwazo katika usajili. Brian anasema bila kuwapo elimu sahihi na endelevu kuhusu masuala fedha, ufikiaji bora wa huduma za kibenki na muundo wa kodi ulio wazi, itakuwa vigumu kwa biashara nyingi kurasimishwa.
Mfumo saidizi na unaotabirika ni muhimu ili kuchochea utekelezaji wa masuala ya kodi. Musa ambaye ni mwanauchumi anayeishi Nyanda za Juu Kusini, anasema hofu ya kodi ya juu kupita kiasi ni kikwazo kingine kikubwa kwa wajasiriamali wasio rasmi wanaohofia urasimishaji kuwawekea mizigo mingi ya kodi na adhabu kali
mambo yanayoweza kuathiri zaidi faida ndogo waipatayo.
Utafiti wa Taasisi ya Financial Sector Deepening Trust Tanzania unaonesha kuwa, wajasiriamali hao wengi hususani wanawake hukabiliwa na unyanyasaji ukiwamo wa matusi na shinikizo kutoka mamlaka za mitaa.
Aidha, madai ya rushwa pia hukatisha tamaa na kuwavunja moyo wajasiriamali dhidi ya utekelezaji wa sheria za kodi. Utafiti uliofanywa na Ilona Steiler mwaka 2018 na kuchapishwa katika jarida la ‘Articulo – Journal of Urban Research,’unabainisha hatari zinazowakabili wafanyabiashara wa mitaani Dar es Salaam kutokana na kuonekana kwao kwa wingi.
Utafiti huo uitwao ‘Kuna nini katika Neno? Dhana ya Siasa ya Biashara Isiyo Rasmi Dar es Salaam,’ unabainisha kuwa, mara kwa mara wafanyabiashara hutozwa faini kali, hufanyiwa unyanyasaji wa kimwili na hata kufunguliwa
mashitaka ya jinai na kuadhibiwa hadi miezi sita jela.
Wakati mwonekano wa waja siriamali hao ukisaidia kuvutia wateja, pia huwaweka katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria. Changamoto hizi huchochea kukosekana imani kwa mamlaka za kodi na kuondoa ari ya ulipaji kodi kwa hiari, hivyo kuongeza pengo kati ya uchumi usio rasmi na uchumi rasmi.
Ili kuondoa vikwazo hivi vya kimfumo, hapana budi yafanyike maboresho ya kodi yenye ufanisi.
Kurahisisha mchakato wa usajili
Jambo la msingi katika maboresho ya msingi ya kodi ili kuimarisha utekelezaji wa kanuni na sheria za kodi ni kurahisisha mchakato wa usajili wa biashara ambao bado ni kikwazo kikubwa kwa wajasiriamali.
John Marwa ambaye ni mtafiti aliyeko Geita, anasema nafasi ya Tanzania ya 141 kati ya uchumi 190 katika ripoti ya Benki ya Dunia ya ‘Doing Business 2020’ inaonesha vikwazo vikubwa vya ukiritimba vinavyozuia urasimishaji wa biashara.
Nafasi hiyo inaonesha ugumu wa taratibu za udhibiti zinazokatisha tamaa wamiliki wa biashara nyingi zisizo rasmi
kuingia katika uchumi rasmi. Hata hivyo, mwaka 2021 Benki ya Dunia ilisitisha Fahirisi ya Urahisi wa Kufanya Biashara.

Kwa mujibu wa Marwa, nafasi ya awali ya Tanzania inadhihirisha hitaji muhimu la kuboresha na kurahisisha
michakato wa usajili na kufanya iwe inayopatikana kirahisi na kwa uwazi kusimamia utekelezaji wa sheria za kodi.
Naye mwanauchumi mstaafu anayeishi katika Kaunti ya Kilifi nchini Kenya, Caleb Abraham anapendekeza mfumo wa usajili uliorahisishwa ujumuishe mfumo wa kodi wa ngazi moja kadiri ya viwango vya mapato ili kuziwezesha biashara zisizo rasmi kufika katika uchumi rasmi.
Anasema kuunganisha mifumo ya usajili na malipo kwa njia ya simu kutapunguza vikwazo vikiwamo vya urasimu, utapunguza ubebaji na matumizi ya karatasi (mafaili) na kusaidia kukabili rushwa sambamba na kujenga mfumo wa kodi wenye uwazi na ufanisi zaidi.
Uanzishaji wa vituo maalumu vya usajili wa kodi katika ngazi ya serikali za mitaa utasaidia kutoa msaada wa moja
kwa moja kwa wafanyabiashara binafsi, utarahisisha mchakato na utabainisha manufaa ya muda mrefu ya urasimishaji.
Profesa mmoja wa Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Makerere (MakSOE) nchini Uganda, anasema kurahisisha
usajili wa kodi ni zaidi ya uimarishaji wa kiutawala na ni zana yenye nguvu ya uwezeshaji wa kiuchumi.
Anafafanua, “Kupitia mfumo ambao ni rafiki kwa watumiaji, Tanzania inaweza kufikia ongezeko la asilimia 40-50 la usajili wa biashara ndani ya miaka mitano hadi saba ijayo, mradi tu kutakuwa na usimamizi thabiti wa sera na msaada.”
Kwa mujibu wa msomi huyo, katika biashara milioni 1.3 iliyosajiliwa sasa, ongezeko la asilimia 50 litaongeza idadi hiyo na kufikia takriban milioni 1.95 hivyo kupanua vyanzo kodi na mapato ya taifa.
Ulipaji kodi kwa awamu
Wachambuzi nchini wanasema mtindo wa ulipaji kodi kwa awamu ni njia ya kisayansi na isiyotisha biashara zisizo rasmi kuingia katika sekta rasmi. Ramadhani Kaniki wa Manyara anasema badala ya kuweka mzigo wote wa kodi
mara moja kwenye biashara, uanzishwe taratibu wa kulipa taratibu madeni ya kodi ili kuzipa kampuni ndogo uwezo wa kumarika kifedha na kukua.
Joyce Mangi wa Arusha Arusha anaunga mkono hoja hiyo akipendekeza mfano wa viwango vya kodi. Anasema biashara ndogo zinazopata chini ya Sh milioni 7 kila mwaka zipewe msamaha wa kodi wa miaka mitatu ili biashara hizo zipate muda na nafasi ya kujiimarisha kabla ya kuanza majukumu ya kodi.
Wakati huo huo, biashara zinazozalisha zaidi ya Sh milioni 7 na si zisizoidi Sh milioni 20 wafaidike kutokana na kupunguza viwango vya kodi katika kipindi cha mpito, hivyo kuwapunguzia mzigo wa kifedha na kuhimiza urasimishaji.
Mchambuzi wa kikanda wa masuala ya uchumi wa Rwanda anasisitiza kuwa, ulipaji kodi kwa awamu utasaidia biashara kuwa na utulivu wa kifedha na kuchochea urasimishaji. Anasema ingawa hakuna takwimu maalumu kuthibitisha athari za moja kwa moja, nchini Rwanda maboresho ya kodi yamechochea utekelezaji wa sheria za kodi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) ya Mwaka 2023, uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa pia umeongezeka maradufu kutoka chini ya asilimia 8 katika miaka ya 1990 hadi zaidi ya asilimia 16 mwaka 2020.
Ripoti ya Wizara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi ya 2023 inasema kujumuisha usajili wa kodi na utoaji leseni za biashara kumepunguza vikwazo vya ukiritimba. Kwa Tanzania, mfumo wa kodi wa awamu utaongeza kasi ya usajili wa biashara kwa asilimia 20-28 katika kipindi cha miaka miwili kutoka usajili wa sasa wa milioni 1.3 hadi katika ya
milioni 1.56 na milioni 1.66.
Ukuaji huu unaweza kuongeza mapato ya kodi kwa asilimia 15-20, ikizingatiwa kuwa biashara mpya huchangia kwa uwiano sawa. Ingawa mafanikio hutegemea utekelezaji na mwitikio wa biashara, maboresho ya Rwanda yanaonesho umuhimu wa kurahisisha taratibu za kodi na usajili ili kuchochea urasimishaji na ukuaji wa mapato nchini.
Hitimisho
Kimsingi, sekta isiyo rasmi ya Tanzania ni nguzo muhimu ya shughuli za kiuchumi, ambayo ujumuishwaji wake katika mfumo wa kitaifa wa fedha unahitaji mbinu za kimkakati, ulipaji kodi wa awamu na maboresho ya kodi.
Kutokana na maoni hayo ya kitaalamu na data, maboresho hayo yanaweza kuongeza utekelezaji wa sheria za kodi, kuongeza mapato ya serikali na kujenga mazingira yanayowezesha biashara ndogo kustawi kwa njia endelevu.
Mbinu ya muundo bora si tu kwamba itaziba pengo kati ya wajasiriamali wasio rasmi na uchumi rasmi, bali itaongeza utulivu wa uchumi muda mrefu.