Ummy atoa siku 14 udanganyifu NHIF

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu,  ametoa siku 14 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kupeleka mpango wa kuboresha takwimu za matibabu,  ambao pia utadhibiti udanganyifu  kwa kutumia  mfumo wa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Amesema hayo leo jijini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari na kueleza kuwa kumekuwepo na vitendo vya udanganyifu kwenye, mfuko huo, hali inayochangia kuyumbisha mfuko.

“Mtuletee mpango ndani ya siku 14, kuboresha takwimu za matibabu, hatutakubali  NHIF itetereke tutachukua hatua, naagiza Katibu Mkuu na timu yako kuhakikisha kunaimarishwa mfumo wa TEHAMA, ili kudhibiti ubadhilifu,” alisema.

Advertisement

Alisema kuwa kuanzia sasa hawatamvumilia mtoa huduma mwenye vitendo vya udanganyifu, kwani  asilimia 70 ya hospitali zinapata fedha kutoka NHIF.

Alisema kuwa baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakifanya udanganyifu na baadhi yao wameshachukuliwa hatua.

Alisema kuwa uwepo wa mfumo wa takwimu za matibabu utapunguza gharama kwa Mfuko.

“Kama mtu alifanyiwa kipimo Bombo kwa nini  afanyiwe tena Muhimbili, mfumo huo ukiwemo utasaidia kuwepo kwa taarifa za mgonjwa kwenye ngazi ya Mkoa ,” alisema.

Pia alisema kumekuwa na udanganyifu kwa wanachama kuwatoa wategemezi na kuwaingiza watu wengine .

“Kuna mwingine anamtoa mtoto kisa haumwi halafu anamuingiza baba mkwe  mgonjwa…. Maana ya Bima ya Afya wengi wanachangia kwa ajili ya wachache  wanaoumwa,” alisema