Umoja wa Mataifa wamuonya mmiliki Twitter

Elon Musk.

UMOJA wa Mataifa (UN) umemuonya mmiliki mpya wa mtandao wa ‘Twitter’ Elon Musk, dhidi ya watumiaji wa mtandao huo watakaochapisha maudhui yenye kuleta chuki na taharuki miongoni mwa watumiaji.

Taarifa ya shirika la habari la Sputnik imemnukuu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric akisema kuwa mtandao huo haupaswi kuwa sehemu ya kueneza maudhui yenye kuleta ubaguzi.

“Tumetangaza kwamba Twitter na mitandao mingine ya kijamii haipaswi kutumiwa kueneza chuki, maudhui yasiyo ya kweli au ubaguzi wa rangi, kwa sababu hiyo tunafuatilia suala hili kwa karibu,” alisema Stephane Dujarric.

Advertisement

Ukurasa wa Umoja wa Mataifa kwenye mtandao wa Twitter wenye wafuasi na watumiaji milioni 16 ni mojawapo ya kurasa zinazotumika sana za mtandao huo wa kijamii, na maafisa wote, idara na ofisi za shirika hilo zina akaunti kwenye Twitter.

Mara baada ya kukamilika kwa makubaliano ya ununuzi wa Twitter, Elon Musk alianza kutimua idadi kubwa ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, suala ambalo limeibua wasiwasi kuhusu sera mpya la mtandao huo.