NOVEMBA 30, 2023 Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ulianza Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Ulianza na mchango wa mfuko wa Upotevu na Hasara utakaosaidia nchi zinazoendelea.
Katika mkutano huo ahadi zilizotolewa ni Sh trilioni 1.3 ambapo UAE imeahidi Sh bilioni 251.5, Ujerumani Sh bilioni 251.5, Uingereza Sh bilioni 127.7, Marekani Sh bilioni 42.7, Japan Sh bilioni 25.15 na Umoja wa Ulaya (EU) Sh bilioni 616.3.
Benki ya Dunia itakuwa mwenyeji wa muda wa hazina hiyo kwa miaka minne.
Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga anasema anazingatia haja ya kujumuisha uwakilishi mzuri wa nchi zilizoendelea (G7) kwenye bodi ya hazina hiyo.
Wajumbe wa Kamati ya Mpito walitoa wito kwa hazina hiyo kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni za UNFCCC na Makubaliano ya Paris.
Mfuko wa hasara na uharibifu utakuwa na sekretarieti inayojitegemea yenye uthabiti wa bodi ya wanachama.
Nchi zinazoendelea zinasema mahitaji halisi yanakaribia Dola za Marekani bilioni 400 kwa mwaka.
Nchi zote zinazoendelea zinastahili kupata rasilimali moja kwa moja kutoka mfuko huo, zikiwa na kiwango cha chini cha asilimia ya mgao kwa nchi zilizoendelea.
Mfuko huo ni ushindi
Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda, akiwa katika mkutano huo anaeleza kuwa kuanzishwa kwa mfuko huo ni ushindi mkubwa kwa wanyonge hasa nchi za Afrika ambazo zilichangia kidogo katika mgogoro wa hali ya hewa.
Anasema mfuko huo ni hatua katika mwelekeo sahihi kwa nchi kama Malawi ambazo zimepata hasara kubwa kutokana na vimbunga vilivyoua zaidi ya watu 500 na kuwakosesha makazi watu 500,000 mwaka huu.
“Tunakaribisha ahadi kutoka kwa mataifa tajiri, lakini tunahitaji maelekezo ya wazi kuhusu jinsi jumuiya zilizo hatarini zaidi zinaweza kufaidika na hazina hii, ambayo lazima pia isifungie nchi katika madeni zaidi, ni wakati ambao ahadi lazima zitekelezwe, tunahitaji hatua na kauli chache zaidi,” anasema Banda.
Anasema tunatumai ahadi za kifedha zitageuzwa haraka kuwa fedha na zitatoka haraka kushughulikia hasara na uharibifu unaohusishwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwani athari haziwezi kusubiri.
Baada ya kufunguliwa rasmi mkutano huo wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi na uchumi wametaka kufanikishwa kwa haraka mfuko wa hasara na uharibifu kwa nchi zinazoendelea kusaidia waathirika.
Wataalamu hao wametaja hatua ya utoaji wa fedha hizo kuwa ni mafanikio makubwa katika mkutano huo kwani mfuko huo ulihitajika muda mrefu.
Kwanini mfuko huo ni muhimu
Akizungumza na HabariLEO, Mkurugenzi wa Powershift Afrika, Mohamed Adow anasema uhitaji wa fedha za haraka ni mkubwa kwa nchi zilizoendelea hasa zile ambazo tayari madhara ya mabadiliko ya tabianchi yameshaonekana.
“Inafurahisha kuona Mfuko wa Hasara na Uharibifu unaanzishwa kwani mwanzoni mwa COP27 nchini Misri watu wengi walisema hautakubaliwa. Hiyo inaonesha jinsi mchakato huu wa UN unaweza kuchukua hatua za haraka kusaidia nchi zinazoendelea.
Anasema japokuwa mfuko huo umepitishwa lakini hakuna sheria zinazousimamia kufanya kazi, hakuna ulazima wa kuchangia mfuko licha ya kuwa mataifa tajiri ndiyo yanasababisha uharibifu huku mataifa yanayoendelea yakiwa katika hatari.
“Ni muhimu Benki ya Dunia kufanya kazi hiyo la sivyo tutahitaji kuanzisha chombo tofauti kufanya kazi hiyo na suala muhimu zaidi sasa ni kupata pesa zinazoingia kwenye mfuko na kwa watu wanaohitaji, tunatarajia viongozi kuahidi fedha hapa kwenye COP28 lakini zisiwe tu ahadi,” anasisitiza.
Anasema fedha zinahitajika kama ruzuku si mikopo kwani mikopo itazidisha madeni kwa nchi zinazoendelea.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Semboja Haji anaeleza nchi zilizoendelea ndio wahusika wakubwa wa mabadiliko hayo hivyo hawana budi kufidia hasara inayopatikana kwa watu wasio na hatia.
“Hatua ya kutoa fedha si tu kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea hata hao walioendelea tunawasaidia, watambue hilo kwa sababu athari inagusa dunia nzima, wasione kama wanatuhurumia sisi. Kitu muhimu ni kuacha kutumia nishati chafu ndio kila kitu kitakaa sawa,” anasema.
Uhitaji ni mkubwa
Profesa Fadhel Kaboub ni mtaalamu wa uchumi na Rais wa Taasisi ya Global for Sustainable Prosperity. Anasema mfuko huo unahitaji kima cha chini cha Dola za Marekani trilioni 2.4 ya uwekezaji wa ruzuku na teknolojia kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ifikapo 2030.
“Kutoa fedha hakuhitaji mikopo, riba wala masharti kwani ni kama wanalipa fidia na haiwezekani mtu unamdai Dola 100 badala yake anakupa mkopo wa Dola 10 wenye masharti ya namna ya kutumia, anakupa Dola 10 nyingine anataka udhibiti wa misitu yako na anakupa Dola 10 tena kwa ajili ya umeme ambao ni lazima umuuzie kwa masharti mazuri, hii si rafiki kwa Afrika hata kidogo,” anaeleza Profesa Fadhel.
Si lengo la mwisho
Mratibu wa Kimataifa wa Mfuko wa Vijana wa Hasara na Uharibifu, Grace Ineza anasema ahadi za hasara na uharibifu zinakaribishwa, lakini hili si lengo la mwisho.
“Tunataka utaratibu wa kifedha ambao unaweza kuhakikisha nchi zinazoendelea zitapata ufadhili wa kutosha, unaotegemea ruzuku na ziada kushughulikia hasara na uharibifu na ahadi zinapaswa kuambatanishwa kwa uwazi jinsi fedha hizo zitakavyodumishwa kwa vizazi,” anasema Ineza.
Naye Mkuu wa Mkakati wa Kisiasa wa Kimataifa wa Climate Action Network International, Harjeet Singh, anasema ni muhimu mfuko wa hasara na uharibifu kipindi cha mwaka baada ya kuanzishwa kwake, kushughulikia masuala ya msingi.
“Kwa upande mmoja, nchi tajiri zimeshinikiza Benki ya Dunia kuwa mhifadhi wa mfuko huu chini ya kivuli cha kuhakikisha majibu ya haraka ya kile kilichojadiliwa COP28, kinyume chake, wamejaribu kupunguza majukumu yao ya kifedha.”
Singh anabainisha kutokuwepo kwa mzunguko maalumu wa kujaza mfuko huo kunazua maswali mazito kuhusu uendelevu wa muda mrefu.
Mshauri Mkuu wa Usimamizi wa Hatari wa Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Germanwatch, Laura Schafer anasema kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuweka msingi wa kusaidia nchi na watu wanaotishiwa na mgogoro wa hali ya hewa katika kukabiliana na athari zisizoepukika za mabadiliko.
Makala haya yamewezeshwa na Mesha na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.
Mwisho