Watu million 6.8 walioko hatarini katika majanga mbalimbali watafaidika na mpango wa Umoja wa Mataifa (UN) wa kupewa msaada, ili kuwanusuru katika katika hali hatarishi wanazokutana nazo.
UN imesema mpango wa misaada ya kibinadamu wenye thamani ya dola bilioni 1.7 umezinduliwa Jumanne huko Sudan Kusini utakaosaidia idadi hiyo ya watu.
Msemaji Mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema kuwa kampeni ya mwaka 2023 inalenga kuwasaidia wahanga wa migogoro, wahanga wa hali ya hewa na wahanga wa kuhama muda mrefu ambao wako hatarini zaidi katika maisha.
Msemaji Mkuu huyo wa Antonio Guterres, vile vile amemnukuu mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Sudan Kusini, Sara Nyanti, akisema kwamba licha ya kuwa mgogoro wa Sudan Kusini unashindana na mambo mengine ya dharura ya kimataifa na kusababisha kupungua sana ufadhili, lakini jamii ya kimataifa inapaswa kuelewa kuwa, watu wa Sudan Kusini wanastahiki zaidi kusaidiwa ili waendelee kuishi.
Stephane Dujarric pia amesisitizia haja ya wafanyakazi wa misaada kulindwa na kuthaminiwa vilivyo usalama wao, ili waweze kuwasaidia wale wote wenye mahitaji hasa wanaoishi maeneo ya vijijini.
Amesema: “Zaidi ya theluthi mbili ya wakazi wa Sudan Kusini watahitaji aina fulani ya msaada wa kibinadamu na ulinzi mwaka 2023.”
Amesema watu milioni 8 wako hatarini kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula katika kipindi cha baina ya Aprili na Julai mwakani.
Aidha Msemaji huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, mpango wa umoja huo wa kudhamini misaada ya kibinadamu wa mwaka huu wa 2022 kwa Sudan Kusini umefadhiliwa kwa asilimia 67 na si wote waliotekeleza ahadi zao.