UN kuyakabili majanga Afrika

Antonio Guterres, United Nations High Commissioner for Refugees speaks during a press conference at the Launch of the Regional Flash Appeal Following recent events in Libyan Arab Jamahiri

ZAIDI ya watu milioni 43 kutoka Ethiopia, Kenya na Somalia wanaendelea kuteseka kutokana na ukame mbaya zaidi katika historia ya miaka ya karibuni uliosababishwa na misimu mitano mfululizo ya ukosefu wa mvua. Umoja wa Mataifa (UN) umeeleza.

Imeripotiwa jitihada mbalimbali zinaendelea kufanywa ili kuzisaidia nchi hizo. Katibu Mkuu Umoja wa Matifa, António Guterres alisema katika hafla ya kukusanya Dola bilioni 7 iliyofanyika Makao Makuu ya Umoja huo huko New York jana.

Miaka mingi ya migogoro na ukosefu wa usalama imesababisha watu wengi kuhama makazi yao, huku bei ya vyakula ikipanda na hivi karibuni, mapigano nchini Sudan, yameongeza hali hiyo. Ilitangazwa baadaye katika siku hiyo kwamba dola bilioni 2.4 zilikuwa zimeahidiwa na wafadhili.

Advertisement

“Lazima tuchukue hatua sasa ili kuzuia mgogoro usigeuke kuwa janga,” Guterres alisema. “Wacha tuchukue hatua kwa pamoja sasa kwa uharaka na msaada mkubwa zaidi.” Aliongeza Guterres.

Hafla ya ahadi hiyo iliitishwa na Umoja wa Mataifa na Italia, Qatar, Uingereza na Marekani, kwa ushirikiano na nchi tatu zilizoathirika.

Katibu Mkuu aliona athari mbaya ya ukame moja kwa moja wakati wa ziara za hivi karibuni nchini Kenya na Somalia.

“Katika sehemu za kaskazini mwa Kenya, mandhari kavu na mifugo iliyoangamia imefukuza familia kutoka katika nyumba zao kutafuta maji, chakula na mapato,” alisema Guterres.

Akiwa katika mji wa Baidoa wa Somalia, alikutana na jamii zilizopoteza maisha kutokana na ukame na ukosefu wa usalama, huku vita dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab vikiendelea.

“Niliguswa moyo sana na mapambano yao. Na nilitiwa moyo na uthabiti wao, ujasiri, na azimio lao la kujenga upya maisha yao. Lakini hawawezi kufanya hivyo peke yao,” aliongeza.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alihakikisha kwamba “hatua italeta mabadiliko yote.” Mwaka jana, wafadhili waliwasilisha msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 20 na kusaidia kuzuia njaa.

Alitoa wito wa kuongezwa msaada kwa mipango ya kibinadamu kwa kanda ambayo kwa sasa inafadhiliwa chini ya asilimia 20.