MAREKANI : BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito kwa kuanzishwa kwa mchakato wa kisiasa wa jumuishi nchini Syria, utakaokuwa unahusisha viongozi na wananchi wa Syria wenyewe, kufuatia kuangushwa kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad.
Katika tamko lake lililotolewa usiku wa kuamkia leo, Baraza la Usalama lilisisitiza kuwa watu wa Syria wanapaswa kupata fursa ya kuamua hatma ya taifa lao na kujenga upya mfumo wa kisiasa kwa njia ya amani, uhuru, na demokrasia. SOMA: Mapigano mashariki ya kati yasitishwe -UN
Tamko hilo pia lilisema kuwa Wasyria na mataifa jirani wanapaswa kuepuka vitendo vyovyote vitakavyoweza kutishia usalama wa kanda ya Mashariki ya Kati.
Tamko hili lilitolewa muda mfupi baada ya Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa kutoa tahadhari kuwa licha ya kuangushwa kwa utawala wa Assad, mzozo nchini Syria haujamalizika.
Balozi huyo alisema kuwa mapigano yanaendelea kaskazini mwa nchi hiyo, hasa kati ya makundi ya Wakurdi na yale yanayoungwa mkono na Uturuki.