UN yataka uchunguzi mauaji Mali

BAMAKO: WATAALAMU huru wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa mamlaka za Mali kufanya uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu madai ya mauaji ya halaiki na kutoweka kwa watu kwa kulazimishwa, wakionya kuwa huenda vitendo hivyo vikawa uhalifu wa kivita au dhidi ya ubinadamu.

Katika taarifa yao, wataalamu hao wamesema wameguswa na tukio la kugundulika kwa miili kadhaa karibu na kambi ya jeshi la Mali wiki iliyopita, muda mfupi baada ya jeshi la nchi hiyo na wapiganaji wa mamluki kutoka Urusi kuwakamata raia kadhaa.

Wameitaka Serikali ya Mali kuhakikisha uchunguzi huo unafanyika bila upendeleo, huku wakihimiza uwajibikaji kwa waliohusika na ukiukwaji huo mkubwa wa haki za binadamu.

Mali, ambayo kwa sasa iko chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021, imeendelea kukumbwa na hali ya ukosefu wa usalama kwa zaidi ya muongo mmoja kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na makundi yenye mafungamano na Al-Qaeda na Dola la Kiislamu.

Tangu kujitenga na ushirikiano wa muda mrefu na Ufaransa, Mali imekuwa ikitegemea usaidizi wa kijeshi kutoka kwa Urusi, hatua ambayo imeibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa kimataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo.

SOMA: Mali yajiondoa mataifa ya Francophonie

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button