UNICEF yatoa mamilioni kukabili mabadiliko ya tabianchi

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetoa Sh milioni 185.429 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maji, Nishati na Madini, Jokha Salum Mohamed.
Alisema mradi huo umelenga kutekeleza mambo manne, ikiwemo upandaji wa miti katika vyanzo vya maji safi na salama Unguja na Pemba. Jokha alisema kumejitokeza tatizo kubwa la uvamizi katika vyanzo vya maji safi na salama, ikiwemo ukataji wa miti iliyozunguka maeneo hayo na hivyo kusababisha tishio la kukauka kwa vyanzo hivyo.
“Tunakabiliwa na uvamizi wa vyanzo vya maji ambapo wananchi wamekata ovyo miti, kiasi cha kutishia kukauka kwa vyanzo hivyo katika kipindi cha kiangazi,” alisema.
Aidha, alisema mradi huo utahakikisha unalinda vyanzo vya maji kwa kujenga uzio ili kuzuia kasi ya watu ya ujenzi wa nyumba za kudumu katika maeneo hayo. Alisema baadhi ya vyanzo vya maji katika maeneo ya Masingini, Mkoa wa Mjini Unguja vimekauka moja kwa moja, kutokana na tabia ya wananchi kuvamia vyanzo hivyo, kujenga nyumba za kuishi, kinyume na masharti ya msitu wa hifadhi ya taifa.
“Umefika wakati wananchi wetu hawaheshimu tena vyanzo vya maji safi na salama pamoja na misitu ya hifadhi ya taifa ambayo wanaivamia na kujenga nyumba za kuishi. Matokeo yake ni kuathiri vyanzo vilivyopo,’’ alisema.
Aidha, aliyataja maeneo ambayo wananchi watanufaika na mradi huo, ikiwemo Donge Mbiji, Wilaya ya Kaskazini Unguja, Kianga, Kaburi Kikombe pamoja na Kiashange Pemba. Alisema kupitia sera mpya ya maji na usafi wa mazingira ya mwaka 2025 idara ya maji, nishati na madini imepewa dhamana ya kusimamia rasilimali za maji nchini, kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa maisha ya binadamu.
“Tunatekeleza sera ya maji na usafi wa mazingira ambayo inasisitiza suala zima la kulinda vyanzo vya maji na uvamizi wake sambamba na mabadiliko ya tabianchi,’’ alisema. Alisema mradi wa UNICEF unajishughulisha na kupambana na mabadiliko ya tabianchi unaotokana na uvumilivu na kulinda vyanzo vya maji na athari zake.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi alitembelea vyanzo vya maji na kubaini uvamizi, ukiwemo ujenzi wa nyumba za kudumu karibu na maeneo hayo na kuzitaka taasisi husika, ikiwemo Mamlaka ya Maji Safi na Salama Zanzibar (ZAWA) kujenga uzio kulinda vyanzo hivyo.



