‘Upimaji matumizi bora ya ardhi utaondoa migogoro’

HATUA ya kuanza utekelezaji wa upimaji wa matumizi bora ya ardhi, imeelezwa itasaidia kuleta amani na utulivu ikiwemo kuondoa migogoro hasa ya wakulima na wafugaji.

Hayo yameelezwa na wananchi wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wakati timu ya wataalamu wa ardhi Mkoa wa Katavi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu walipofika na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Mishamo juu ya azma ya serikali kutekeleza mpango huo.

“Tumefarijika na wenzangu na ujio wenu kuja kutuwekea huu utaratibu, bila shaka itaepusha mambo mengine ambayo yalikuwa yanatukosesha amani na utulivu kwa kuwa mtakuja kutenga sehemu ya kilimo, sehemu za ufugaji, watu wote tutaishi kwa amani na utulivu bila migogoro,” amesema kwenye mkutano huo Ndayegamiye Seth mkazi wa Mishamo.

Kwa upande wake Ibrahim Butta, Ofisa Mipango Miji Mkoa wa Katavi, amesema mpango wa matumizi bora ya ardhi una manufaa kwa wananchi kwa kuwa serikali hupeleka miradi sehemu yenye mpangilio mzuri wa ardhi na pia ni wajibu wa serikali kuhakikisha wananchi wake wanaishi katika mpangilio unaoeleweka.

Amesema mpango huo unasimamiwa na wananchi wenyewe wakiwaongoza wataalamu kwa kuwa wao ndio wenye kuijua mipaka na kupendekeza matumizi ya ardhi katika eneo lao na amewaomba wananchi kutoa ushirikiano pale wataalamu watakapopita kutoa elimu na kupata taarifa mbalimbali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa suala la mipango bora ya ardhi ndio ufunguo wa maendeleo duniani kote, kwani bila mpango huo migogoro itaendelea kuwepo na kusababisha kukwamisha maendeleo.

Ametoa wito kuwa makundi yote kushirikishwa katika tukio zima la upangaji, huku akiwaonya wote watakaobainika kuhujumu mpango huo.

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Nehemia James amesema kutokana na umuhimu wa suala hilo, tayari Serikali ya Mkoa imeshapata baraka kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na utekelezaji wake utafanyika maeneo ya makazi ya wakimbizi ya Mishamo na Katumba

Habari Zifananazo

Back to top button