URUSI : MAMIA ya wafungwa wa Urusi na Ukraine wameachiliwa huru kupitia mpango wa kubadilishana wafungwa uliosimamiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky amethibitisha hilo na kusema kuwa wafungwa 189 wa Ukraine, wakiwemo maafisa wa kijeshi, walinzi wa mpaka na walinzi wa kitaifa pamoja na raia wawili, wameachiwa.
Huku Wizara ya Ulinzi ya Urusi nayo ikithibitisha na kusema kuwa askari 150 wa Urusi wameachiliwa huru kama sehemu ya ubadilishanaji huo ambao kila upande uliwaachia watu 150.
Hatahivyo, taarifa haikuweza kuanisha kuwa idadi ya wafungwa wa Ukraine walioachiliwa walikuwa zaidi ya 150. SOMA: Vita ya Urusi ‘ilivyomhamishia’ raia wa Ukraine kijijini Kizimkazi-Unguja
Utaratibu huu wa kubadilishana wafungwa kati ya Urusi na Ukraine umekuwa ukifanyika katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanza kwa vita vyao.
Urusi imesema askari wake kwanza walipelekwa kwenye mpaka wa jirani yake Belarus, ambako walipewa msaada wa kisaikolojia na matibabu kabla ya kupelekwa Urusi.