KATIKA kuhakikisha uchumi wa bluu nchini unazidi kukua, Shirika la misadaa la Marekani ‘USAID’, limetangaza kuiongeza fedha Tanzania katika mradi wa Heshimu Bahari kutoka Dola za Marekani milioni 13 hadi Dola milioni 25 sawa na Sh bilioni 62.525.
Mkurugenzi wa Misheni wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania, Craig Hart ametangaza uamuzi wa kuongeza fedha hizo leo Oktoba 26, 2023 katika Maadhimisho ya Miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) yaliyofanyika katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Amesema nyongeza hiyo imetokana na mazungumzo ya Balozi wa Marekani na Wizara ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar na Wizara ya Mifugo ya Tanzania Bara, yaliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu.
Amesema fedha hiyo itaongeza maeneo ya mradi huo kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za uvuvi na utunzaji wa rasilimali za bahari.
Maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Mwambao wa Bahari ya Hindi Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, Mafia, Kilwa na Mnazi Bay Ruvuma.
Amesema mradi huo wa ‘Heshimu Bahari’ ni wa miaka mitano unakwenda kuisaidia Tanzania katika maendeleo ya uchumi wa bluu.
Amesema, sehemu ya fedha hizo ni ruzuku itakayowawezesha wananchi wanaoishi maeneo yanayoizunguka bahari, kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali.
Craig amesema pia mradi wa Hashimu Bahari unajikita katika kuimarisha sera zitakazosaidia serikali ya Tanzania, sekta binafsi pamoja na jamii kwenye kuimarisha, kuhifadhi, matumizi endelevu ya rasilimaliza bahari.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (ZAFIRI), Zakaria Ally Khamis amesema sehemu kubwa ya mradi huo ni kushirikiana na sekta binafsi kupitia kwenye mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya bahari ikiwa ni pamoja na mazao ya mwani, jongoo bahari, kwani kwa tafiti mbalimbali wametambua ua maeneo yanayohitaji msadaa.
Pamoja na hayo ameeleza kwamba watahakikisha wanawajengea uwezo vikundi vya kina mama pamoja na vijana kwa kuwapatia ruzuku kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji kwa ajili ya maendeleo ya bahari.
Comments are closed.