Ushahidi kesi ya Kisena kuanza Sept 7

Ushahidi kesi ya Kisena kuanza Sept 7

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi inatarajia kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Robert Kisena na wenzake watatu.

Ushahidi huo utaanza kusikilizwa Septemba 7, mwaka huu na upande wa mashitaka ukisema una mashahidi 24 na vielelezo 60.

Hayo yalielezwa mahakamani baada ya Wakili wa Serikali, Timotheo Mmari kuwasomea washitakiwa hao mashitaka upya mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.

Advertisement

Washitakiwa wengine ni Mkurugenzi wa UDA, Charles Newe, mfanyabiashara, John Samangu na Mtunza fedha wa UDART, Tumaini Kulwa.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 15 yakiwamo kuisababishia UDART hasara ya Sh milioni 750, kuongoza genge la uhalifu, utakatishaji fedha haramu, kuwasilisha nyaraka za uongo na kughushi.

Katika shitaka la kuongoza genge la uhalifu, washitakiwa hao walidaiwa katika nyakati tofauti kati ya Mei 25 na Julai 10, 2016 katika maeneo tofauti Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh milioni 750 kutoka akaunti ya UDART Tawi la Bank House NMB.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kughushi, mawili ya kuwasilisha nyaraka za uongo na mashtaka tisa ya utakatishaji fedha haramu.

Katika mashitaka ya kughushi ilidaiwa Mei 26, 2016 Dar es Salaam kwa udanganyifu na kwa makusudi walighushi fomu inayoitwa ya kuhamisha fedha wakionesha UDART imehamisha Sh milioni 750 kutoka katika akaunti yake iliyoko Benki ya NMB kwenda akaunti inayomilikiwa na Kampuni ya Longway Engineering Ltd iliyoko Benki ya KCB za ujenzi wa vituo vya mabasi na uzio Kimara, Kivukoni, Ubungo na Morocco, wakati wakijua si kweli.

Washitakiwa hao walikana mashtaka hayo, lakini walikiri taarifa zao binafsi baada ya kusomewa hoja za awali.

Kisena alikubali majina yake na kwamba ni Mkurugenzi wa UDART, Mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil and Gas na Mkurugenzi wa Simon Group.

Mshitakiwa Newe alikubali majina yake na kuwa ni Mkurugenzi wa UDA, Shirika la Usafiri Dar es Salaam na Samangu yeye alikiri majina yake na pia alikiri kuwa ni mtia saini wa Zenon Oil and Gas, huku Kulwa akikubali majina yake na ni mwajiriwa wa UDART akiwa mtunza fedha.

Baada ya maelezo hayo upande wa utetezi ambao ulikuwa na mawakili wanne wakiongozwa na Nduruma Majengo, waliomba kupewa muda ili wawasilishe idadi ya mashahidi na vielelezo vyao.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Luvanda alikubaliana na ombi hilo na kuwataka wawasilishe idadi ya mashahidi na vielelezo Septemba 9, mwaka huu. Washitakiwa walirudishwa rumande.