Ushirikiano wa PURA, ZIPRA wamkosha Katibu Mkuu

DAR ES SALAAM: Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Kepteni Hamad Bakar Hamad (wakwanza kulia) amezipongeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) kwa kuendeleza mashirikiano ya kisekta.
Kept. Hamad ametoa pongezi hizo leo, Julai 07, 2025 alipotembelea banda la PURA wakati wa maonesho ya 49 ya Saba Saba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
SOMA: Ushirikiano PURA, ZPRA unavyokuza sekta ya mafuta, gesi asilia|
Akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu, mjiolojia mwandamizi wa PURA, Ebeneza Mollel, alisema tangu kusainiwa kwa hati ya ushirikiano kati ya PURA na ZPRA mwaka 2022, taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo.
Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na usimamizi wa taarifa za petroli, ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uandaaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali.
Maeneo mengine ni udhibiti na usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli na ushiriki wa wananchi katika shughuli hizo
“Nitumie fursa hii kukujulisha kuwa taasisi hizi zimeendelea kutekeleza Hati ya Mashirikiano na wiki iliyopita, Julai 01, 2025, menejimenti ya PURA na ZPRA zimefanya kikao cha sita kujadili taarifa ya utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano kwa mwaka 2024/25” alieleza Ebeneza.
Baada ya kupewa maelezo hayo, Hamad alitoa pongezi kwa namna ambavyo PURA na ZPRA zimeendelea kushirikiana na kutoa rai kwa taasisi hizo kuyaenzi mashirikiano hayo.