Usinunue ardhi kabla ya uhakiki halmashauri-Mabula

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amewataka wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za halmashauri.

Mabula alisema hayo wilayani Kibaha Alhamis alipokwenda na Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Mashimba Ndaki kupokea na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa ardhi katika eneo la kiwanja namba 34 Pangani Kibaha chenye ukubwa wa hekta 1,037.

Wananchi 1,002 wamebainika kuvamia kiwanja cha eneo hilo linalomilikiwa na  Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya taasisi yake TVLA.

Katika uchunguzi wake, kamati ilifanikiwa kuwahoji wananchi wavamizi 1,156 katika mitaa ya Kidimu, Lumumba na Mkombozi.

Kamati ilisikiliza, kuwahoji na kupokea vielelezo mbalimbali kutoka kwa wananchi 1,002 waliovamia eneo. Kati ya hao, wavamizi 154 hawakuwa na nyaraka zozote za namna walivyopata maeneo kwenye eneo hilo.

Akisoma taarifa ya kamati ya uchunguzi, Katibu wa Kamati ambaye ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani, Husein Sadick, alisema katika mahojiano na wananchi hao, 403 walikiri kuvamia kwa kujikatia vipande vya ardhi.

Wananchi 46 walidai kupewa vipande vya ardhi na wavamizi waliotangulia na wananchi sita walidai walirithi maeneo hayo. Hata hivyo, watu hao waliovamia eneo wamefanya maendelezo pasipo kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri kama taratibu zinavyoelekeza.

Kwa mujibu wa Sadick, historia ya eneo hilo ilianza 1982 kwa wizara kuomba eneo la kuzalisha mitamba kwa ajili ya kuhudumia Kanda ya Mashariki na hekta 4,000 kutwaliwa huku wananchi waliokuwa wakiishi eneo hilo walilipwa fidia kwa awamu tofauti.

“Eneo lilipatikana kihalali na wizara na mwaka 2007 wananchi walivamia ambapo tathmini ya kamati ilibaini uwepo nyumba zilizojengwa kwa tope au mabati, nyumba zisizokamilika au chumba kimoja pamoja na zile zenye makazi,” alisema Sadick.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Lumumba Kata ya Pangani Kibaha mkoani Pwani, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Mabula alitoa rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za halmashauri na kufuatilia kufahamu maeneo yaliyo na hati.

”Nitoe rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za halmashauri na kufanya research kwa maeneo yaliyo na hati,” alisema Mabula.

Akielezea mgogoro katika eneo la Pangani, Waziri wa Ardhi alieleza kuwa, ilibainika uwapo wa wavamizi waliounda magenge ya kutapeli wageni kutoka nje ya Kibaha hasa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na kujifanya wamiliki wa asili katika maeneo waliyovamia.

Waziri wa Ardhi alielekeza wananchi wote waliouziwa ardhi ndani ya Kiwanja Na. 34 Pangani kuwafungulia mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wale wote waliowauzia ardhi pamoja na walioshirikiana nao kufanya mauzo hayo.

Pia alitaka watu hao waliovamia, waliotumia au kuandaa nyaraka za kughushi wachukuliwe hatua za kisheria kwa kusababisha uvamizi kwenye maeneo yenye miliki za watu wengine.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ndaki alisema amefurahi mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na taasisi iliyo chini ya wizara yake kufikia mwisho. Alishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuunda tume ya kuchunguza suala hili.

“Naipongeza timu ya uchunguzi kwa kueleza ukweli na ukweli unapendwa na watu wachache na nakubaliana na mapendekezo yote ya timu ya uchunguzi,” alisema Ndaki.

Ndaki alisema wizara ina huruma maana pamoja na kumiliki kihalali hekta zote  4,000 lakini bado imeamua hekta 2,963 kati ya hizo ziende halmashauri na wao kubaki na hekta 1,137.

Waziri Ndaki aliagiza kuchukuliwa hatua kwa yeyote atakayevamia tena eneo lililobaki huku akisisitiza mipaka ya eneo lililobaki iainishwe na kulindwa ili kuepuka uvamizi mwingine.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alisema uongozi wa mkoa wake utasimamia na kutenda haki wakati wa utekelezaji mapendekezo ya tume ya uchunguzi na kusisitiza haki itatendeka.

Mkoa wa Pwani umekuwa na migogoro mingi ya ardhi iliyosababisha waziri wa ardhi kuunda kamati ya uchunguzi kubaini wavamizi walivyopata ardhi, kubaini matapeli wote waliohusika kuuza ardhi na kisha kuishauri serikali kuchukua hatua stahiki.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button