Utafiti: Asilimia 70 biashara mpya zinakufa

DAR ES SALAAM; UTAFITI unaonesha zaidi ya asilimia 70 ya biashara zote mpya zinazoanzishwa kila mwaka zinakufa kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo uongozi na usimamizi mbaya wa biashara zinazoanzishwa.

Meneja wa Benki ya NBC, Tawi la Mlimani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), Anne Mwaisaka amesema hayo alipokuwa akifunga mafunzo kwa wajasiriamali wanawake yaliyoandaliwa na benki hiyo kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema pia tafiti hizo zinasema, wanawake wengi biashara zao zinakufa kutokana na kukosa mwongozo na uelewa mkubwa na mzuri wa kushindana kibiashara pale wanapoanzisha biashara.

Mwaisaka amesema pamoja na kukosa mwongozo kwa wanawake hao, idadi kubwa  wakuwa na ujasiri wa kuanzisha biashara.

“Tulipopata maombi kutoka UDSM juu ya mafunzo haya, kwetu kama benki ilikuwa habari njema, lakini pia ikawa habari njema kwa wateja wetu maana watapata mafunzo haya na hivyo kuweza kukuza biashara zao kwa kutumia ujuzi watakaoupata kupitia mafunzo haya,” amesema.

Amesema mafunzo waliyopata yamelenga kuwajengea wanawake ufahamu wa aina mbalimbali za biashara na usimamizi mzuri, ikiwa ni pamoja na kuwajengea ujuzi utakaowawezesha kuwa na ubunifu.

Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka chuoni hapo, Profesa Goodluck Urassa, amesema wanawake 36 wamehitimu mafunzo hayo.

” Wanawake wana ubunifu wa hali ya juu, wana biashara zinazoweza kukua na ni wapambanaji,” amesema.

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, upande wa utafiti Profesa Nelson Boniface amesema mwelekeo wa chuo hicho ni kujiunganisha na taasisi binafsi na serikali ili kuwe na mabadiliko chuoni hapo.

Habari Zifananazo

Back to top button