Utafiti Costech wawapa raha wafugaji Kongwa

‘UNAPOMNENEEPESHA mnyama kitu cha kwanza kama mfanyabiashara, unategemea kuongeza uzito wa mnyama na kuongeza thamani ya mnyama mwenyewe anayechinjwa.

“Pia kuongeza ubora wa nyama yenyewe kutokana na ng’ombe aliyenenepeshwa,,” hiyo ni kauli ya Meneja wa Ranchi ya Kongwa iliyopo Dodoma, Elisa Binamungu anasema wakati wa ziara ya watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), walipotembelea ranchi hiyo.

Anasema ng’ombe aliyenenepeshwa na yule ambaye hakunenepeshwa akichinjwa nyama yake itakuwa na ubora tofauti.

Maelezo ya Binamungu, yanaungwa mkono na Ofisa Ugani wa Kata ya Mtanana, iliyopo Wilaya ya Kongwa Dodoma, Dominica Swa, anayesema kupitia mradi wa unenepeshaji ng’ombe uliopelekwa katika kata yao na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Sebastian Chenyambuga, umetoa matokeo chanya.

“Kuna mifugo ilifugwa ndani ya miezi mitatu ambapo mfugaji aliingiza katika banda ikiwa na kilo 160 ama 200, lakini baada ya muda mifugo iliongezeka sana ndani ya miezi mitatu,” anasema.

Maelezo ya Swai ni kwamba kata hiyo ilikubali kufanyika kwa utafiti huo wa unenepeshaji wa ng’ombe ambao ulisimamiwa na Profesa Chenyambuga kutoka Idara ya Sayansi za Wanyama, Ukuzaji Viumbe Maji na Nyanda za Malisho SUA.

Profesa Chenyambuga anataja jina la Mradi huo ni ’Kuboresha uzalishaji wa nyama kutoka kwenye ng’ombe wa kienyeji,’ ulianza 2019 na kukamilika 2022.

Anasema lengo la mradi la kwanza ilikuwa ni kutengeneza chakula cha gharama nafuu kinachotokana na vyakula vilivyopo maeneo ya vijijini kwa ajili ya kunenepeshea ng’ombe wa kienyeji.

Chakula ambacho kitakuwa na virutubisho stahili kwa kuwa vinavyouzwa madukani, gharama yake ni kubwa.

“Huko nyuma wizara ya mifugo walijaribu kunenepesha pale Mtibwa, wakatengeneza chakula lakini cha gharama kubwa. Kwa mfano kinatumia mahindi halisia na molasesi kwa hiyo gharama yake ikawa kubwa.

“Utafiti ule unaonyesha kwa kutumia chakula kile huwezi ukapata faida labda kama bei ibadilike. Tukaja na wazo tutengeneze chakula cha bei rahisi lakini kina virutubisho vinavyostahili na ubora unaofaa lakini kwa kutumia vyakula ambavyo vipo kule vijijini,” anasema.

Anasema lengo la pili lilikuwa kuboresha utumiaji wa mabua ya mahindi au mpunga yaweze kutumika kulishia ng’ombe.

“Baada ya kuvuna mahindi au mpunga watu wanachungia tu kule lakini njia bora ya kutumia hayo mabua badala ya kuchungia kule tuyatengenezee chakula kwa ajili ya kunenepeshea ng’ombe,” anasema na kuongeza kuwa lengo la tatu ni kuangalia fursa ya soko iliyopo kwenye nyama ya kienyeji.

“Hapa ni kwa kuwezesha wafugaji wa ng’ombe wa asili ili kuwaunganisha kuanzisha vikundi vya unenepeshaji wa ng’ombe na kuwaunganisha na soko na taasisi za fedha.

“Sasa hivi mtu anapouza ngombe anapeleka mnadani hanenepeshi, anapeleka aliyekonda kwa hiyo wanapata bei ya chini hivyo tulitaka kuingiza wazo kuwa kabla ya kuuza mtu anenepeshe ng’ombe ndipo amuuze. Mkiwa na kikundi ndio mtaongeza uwezo wa kusambaza,” anasema.

Maelezo ya Profesa huyo, katika utafiti wake walitumia pumba za mahindi na za mpunga pamoja na molasesi, waliongeza madini na chumvi kwa ajili ya kutengeneza vyakula vya kunenepesha vya aina nne.

Utafiti huo ulishirikisha wafugaji wa eneo la Kongwa kwa kufanya unenepeshaji huo kwa sababu waligundua hawana elimu hiyo, na kuchagua kijiji cha Mtanana A na Mtanana B kwa kuwa vipo barabarani, kuwawezesha jamii kuona kuna jambo linaendelea.

Kupitia wakulima hao wa Kongwa, awamu ya kwanza walianza na ng’ombe 50 kwa kuchukua wale wa miaka miwili mpaka mitatu kwa kuwa bado hawajakomaa nyama yao huwa ni laini.

“Katika ng’ombe hawa 50 walioletwa na wakulima tuliwatenga kundi la kwanza walichunga, kundi la pili lilikuwa na vyakula vya aina nne, tulichukua hao ng’ombe 50 tukawapa utambulisho wakakaa kwa siku 90 .

“Kulikuwa na majani makavu na chakula kilichotengenezwa cha ziada. Chakula kingine kilitumia pumba, molasesi na mashudu ya alizeti,” anasema.

Anasema matokeo ya mradi huo uliwawezesha  wakulima hao kutengeneza faida ya kati ya sh 160,000 mpaka 250,000. Chakula walichotengeneza kiliwapa faida kubwa na ng’ombe waliweza kuongezeka uzito kwa haraka zaidi.

Awamu ya pili ya ufugaji waliweza kukata majani mwezi wa tano na wa sita kabla ubora wake haujapotea, kisha walitengeneza mikate kwa ajili ya ng’ombe. Walitumia mabua ya mpunga badala ya majani, walivundika kwa kushindilia chini.

“Tuliona kutumia mabua ya mpunga kuchanganya na urea kuvundika kwa siku 21 ng’ombe ataongezeka uzito kwa haraka,” anasema.

Baada ya kunenepesha mifugo hiyo anasema waliweza kuingia ubia na ranchi ya taifa (NAFCO), na kuuza mifugo yao huko.

Maelezo ya mtafiti huyo ni kwamba serikali kupitia Costech imemwezesha kupata sh milioni 120 katika mradi huo.

Kwa upande wa Kikundi cha Muungano Mtanana ambacho kilishiriki katika mradi huo, Katibu wake Amon Chizuwa anakiri kwamba mradi huo umewapatia manufaa makubwa kwa kuwa kabla hawajawapeleka ng’ombe wao katika mradi huo walikuwa na uzito wa chini, lakini matokeo yake baada ya kunenepeshwa yalionekana dhahiri.

Kuhusu ranchi ya Kongwa, Meneja Binamungu anasema ipo chini ya Kampuni ya Ranchi ya Taifa.

Kwamba ranchi hiyo inajihusisha na ufugaji wa mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na farasi. Na eneo lote ukubwa wake ni hekta 38,000.

Kati ya hizo hekta hizo, zimegawanywa hekta 18,430 vitalu vidogo  na kupewa wananchi waendeleze ufugaji.

Kwa ranchi wanayoisimamia imebaki na hekta 19,570 na ndani ya eneo hilo kuna jumla ya ng’ombe 12,000, kondoo 800, na farasi.

Anasema kupitia mradi wa Costech wa unenepeshaji ng’ombe kwa awamu zote mbili walizofanya waliinunua mifugo hiyo kwa kuwa ilinenepeshwa na kuongezeka uzito.

“Gharama za unenepeshaji ilikuwa gharama za kawaida. Na baada ya kunenepeshwa mifugo iliuzwa kwao kwa kilo. Tulinunua kilo moja hai kwa sh 3000.

“Kwa bei waliyouzia hapo walipata faida kubwa, na wao walionunua walipata faida kubwa, kwa hiyo uwepo wa wanenepeshaji ambao ni wafugaji waliowazunguka katika hilo eneo ni fursa kubwa kwao.

“Na hivi sasa tulikuwa tumepewa malengo makubwa sana ya kuuza nyama tani 50,000 kwa mwaka lakini ukiangalia uwezo wa mifugo tuliyonayo sisi wenyewe hatuwezi kutoa tani 50,000,” anasema.

Anaongeza kuwa ili waweze kutoa kiasi hicho kikubwa cha nyama lazima washirikiane na hao wafugaji wadogo.

Na ili wafugaji wadogo wafanye vizuri nao wanahitaji ufadhili kwa hiyo, “Niendelee kuomba costech muendelee kufadhili wafugaji, muongeze idadi ya vikundi na si kikundi kimoja,”.

Maelezo yake ni kwamba, ukimnenepesha ng’ombe kila siku anaweza kuongezeka kati ya gram 500 mpaka 1000. Maana yake kwa miezi  mitatu atakuwa ameongezeka kati ya kilo 45 mpaka kilo 90.

“Ukijumlisha na uzito anzilishi alioanza nao kati ya kilo 180 au 200 maana yake mpaka unamchinja atakuwa amefikia kilo kuanzia kilo 230 mpaka 250 nusu yake ukimchinja unapata nyama, ukimchukua ngombe ambaye ana umri mkubwa Zaidi wakati wa unenepeshaji, yule ng’ombe atanenepa hataongezeka sana nyama lakini atajaza mafuta,” anasema.

Ofisa kutoka Costech, Mwela anaeleza kuwa tume hiyo inahakikisha utafiti, ubunifu unatoa mabadiliko makubwa na ndio maana serikali inatoa fedha kuhakikisha tafiti zinafanyika.

“Tunataka tafiti zibadilishe maisha ya watu kiuchumi,” anasema.

Habari Zifananazo

Back to top button