UTAFITI umebaini chanjo ya kukinga samaki aina ya sato dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na bakteria.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Morogoro, Dk Alexander Mzula amesema hayo alipozungumza na HabariLEO katika maonesho ya Nanenane kitaifa yanayoendelea mkoani Mbeya.
Dk Mzula amesema samaki hao huugua hasa wanapokuwa kwenye hatua ya vifaranga kwa kuvilia damu na kutoka vidonda.
“Ugonjwa huu ukiingia kwenye bwawa unaweza ukaua mpaka asilimia 100 ya samaki. Sasa kutibu ni ngumu na miongozo yetu hairuhusu kutumia dawa za antibayotiki kwenye mabwawa,” amesema.
Amesema kwa sasa chanjo hiyo ipo katika hatua za mwisho kupitia ufadhili wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ikishirikiana na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela pamoja na SUA.
Amesema utafiti wa awali unaonyesha chanjo hiyo inaweza kukinga kufikia asilimia 90 ya samaki wakawa hai.
Amesema chanjo hiyo ni ya kuogesha, hivyo inaweza kuchanja samaki wengi zaidi kwa mara moja.
Comments are closed.