UTAFITI: Wananchi hawatambui kamati usimamizi vituo vya afya

UTAFITI umebaini kuwa asilimia kubwa ya wananchi hawajui kama kuna Kamati za Usimamizi wa Vituo vya Afya pamoja na Bodi za Afya za Halmashauri zinazosimamia utoaji wa huduma za afya kwa vituo vya afya na hospitali za wilaya nchini.

Mtafiti kutoka Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Stephen Maluka amesema hayo alipozungumza na HabariLeo.

Profesa Maluka amesema kama wananchi hawajui kuna kamati na bodi hizo maana yake ni kwamba uwajibikaji wake pia ni chanagamoto.

Amesema kutokana na uelewa wa wananchi kuwa mdogo utafiti ulionyesha kuwa asilimia 96.7 hawajawahi kupata mrejesho wowote kutoka kwenye hizo kamati hilo linadhihirisha kuwa uhusiano kati ya Kamati, bodi na wananchi ni mdogo.

“Matokeo ya utafiti yanaonesha wananchi wengi hawana uelewa kuhusu kazi za Kamati za Usimamizi wa Vituo vya Afya na Bodi za Afya nchini.

“Asilimia 85.3 ya wananchi walikuwa hawajui kama kuna Kamati za Usimamizi ya Vituo vya Afya. Na asilimia 96.5 walikuwa hawajui kama kuna Bodi ya Afya ya Halmashauri,” amesema.

Ameongeza kuwa asilimia 88.3 hawakuwahi kusikia kuhusu uchaguzi wa wajumbe wala kushiriki kuwachagua wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Vituo vya Afya na Bodi ya Afya ya Halmashauri.

Ametaja malengo ya utafiti huo kuwa ni kutathimini uelewa wa wananchi kuhusu utendaji kazi wa Kamati za Usimamizi wa Vituo vya Afya na Bodi za Afya za Halmashauri,

Pamoja na Kutathimini Uwajibikaji wa Kamati za Usimamizi wa Vituo vya Afya na Bodi za Afya za Halmashauri zilizopo nchini.

Ameeleza lengo lao kwenye utafiti huo ni kuona namna gani Kamati za Usimamizi wa Vituo na Bodi za Afya za Halmashauri zinaweza kuimarishwa ili zisimamie vizuri rasilimali watu na fedha kwenye Vituo vya Afya nchini.

Utafiti huo ulihusisha Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya na Halmashauri ya Mji wa Handeni Mkoa wa Tanga, ulifanyika kati ya mwezi Julai na Oktoba mwaka jana.

Utafiti huo uliwashirikisha wananchi 1184.

Mwisho

Habari Zifananazo

Back to top button