TANZANIA inatarajia kunufaika kiuchumi utakaotokana na kukuza utalii wa mikutano na matukio (MICE Tourism) na kutangaza utalii kimataifa wakati itakapokuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali wa Afrika (AAAGs) unaotarajia kufanyika Desemba 2 hadi 5, mwaka huu mkoani Arusha.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude amesema hayo Novemba 7,2024 mjini Morogoro alipowasilisha mada kwenye Kongamano kati ya Wizara ya Fedha na wahariri wa vyombo vya habari nchini.
CPA Mkude amesema mkutano huo wa kimataifa utafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) na unatarajiwa kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema mkutano huo pia utaudhuriwa na Rais wa Shirika Fedha la Kimataifa (IMF), Pan African Federation Of Accountants(PAFA), pamoja na Washirika wa Maendeleo wa Kimataifa.
Ametaja faida za mkutano huo wenye kushirikisha washiriki zaidi ya 2,000 ukihusisha pia watalaam wa masuala ya Tehema, maofisa ugavi serikalini, wa kampuni binafsi na waliojiajiri.
CPA Mkude amesema pia utatoa Jukwaa la kuwasilina na maofisa wa ngazi za juu za serikali pamoja na washirika wa Kimataifa.
“ Tunatarajia kupokea ugeni mkubwa na nidhahiri kuwa wafanyabiashara wa nyumba za wageni, usafiri ,mama lishe na jamii kwa ujumla watafaidika kiuchumi na kijamii,”amesema CPA Mkude.
“ Tunatarajia wageni kutoka nje ya nchi watakuja na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa nchini kwa kuunga mkono dhamira ya rais ya kutangaza utalii wa tanzania,na wageni hao watatembezwa kwenye mbuga za wanyama na vivutio mbalimbali vya utalii” amesema.
Amesema wageni hao wakiwa hapa nchini watatembelea vivutio vya utalii ambavyo ni Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Duluti, Hifadhi ya Taifa ya Arusha na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
CPA Mkude,ametaja faida nyingine ya mkutano huo kwa Tanzania ni pamoja na Afrika yenye mafanikio yenye msingi ya ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, bara jumuishi lililounganishwa kisiasa na kwa kuzingatia maadili ya Pan –Africanism na maono ya mwamko wa Afrika.
Manufaa mengine ni kuwa na Afrika yenye Utawala bora, Demokrasia, kuheshimu hakiza binadamu na utawala wa sheria, Afrika yenye amani na usalama pamoja na kuwa na afrika yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja, maadili na maadili yanayoshirikishwa.
Umoja wa Wahasibu Mkuu wa Serikali wa Afrika ulizinduliwa rasmi Mombasa, Kenya, Julai 5, 2023 baada ya Azimio la kufunga Umoja wa Wahasibu Wakuu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika (ESSG) pamoja na Jumuiya nyingine za Wahasibu wakuu wa Afrika zilizokuwepo katika Kanda mbalimbali.
Mkutano wa AAAGs unafanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake Julai,5,2023 ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika nchini Lesotho ambapo kwa sasa nchi 57 za Umoja wa Afrika ni Wanachama wa Umoja huo.