Utekelezaji ujenzi shule za michezo waiva

DODOMA; SERIKALI imesema zabuni ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule za michezo imetangazwa ili kupata mkandarasi.
Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini leo mei 25,2026 na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kusini, Moses Kaegele aliyehoji serikali ina mpango gani wa kujenga shule za michezo kwa kila jimbo hasa katika Jimbo la Nkasi Kusini, ili kuibua vipaji vya wanasoka nchini.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri Mwinjuma, amesema serikali imedhamiria kujenga shule 56 za michezo katika mikoa yote nchini, ambapo baada ya kukamilika kwa shule hizo kila mkoa unatarajiwa kuwa na shule za michezo angalau mbili.
“Katika kutekeleza mpango huo serikali imeanza na shule saba za michezo katika mikoa ya Singida, Tanga, Ruvuma, Pwani, Dodoma, Kagera na Mtwara ambapo zabuni ya utekelezaji wa mradi huo tayari imetangazwa, ili kupata mkandarasi wa mradi husika.
“Kukamilika kwa shule hizo kutasaidia kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo mbalimbali, huku wakipata fursa ya kuendelea na masomo,” amesema Naibu Waziri.
Amesema katika awamu zinazofuata za utekelezaji wa mradio huo, Mkoa wa Rukwa utafikiwa na unatarajiwa kunufaika kwa kuwa na shule mbili za michezo ambazo zitasaidia kuibua vipaji vya michezo mbalimbali ikiwemo soka.



