UTPC waanzisha kampeni dhidi ya ukatili wanawake, watoto

UMOJA wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC) umeanzisha kampeni maalum ya siku 16 kutoa elimu kwa jamii ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia  kwa kundi la  wanawake na watoto.

Kampeni hiyo maalumu inashirikisha  zaidi ya waandishi wa habari 1,000 nchini na inalenga kushirikiana na Serikali kwenye mapambano ya kuzuia vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa ni janga kwa taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC,  Kenneth Simbaya, alisema hayo mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo maalum .

Simbaya alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto ni miongoni mwa ukiukwaji  uliokithiri wa haki za binadamu .

Kampeni ya mwaka huu imebeba kauli mbiu inayoleza wekeza, zuia ukatili wa kijinsia.

Simbaya alisema vyombo vya habari vikiandika habari hizo za kutoa elimu kwa jamii kwa ajili ya kuzuia vitendo vya ukatili kwa makundi hayo vitasaidia kuleta mjadala mpana kwenye jamii na jinsi wanavyojadilina ndio kutaleta mabadiliko.

“ Tukilifanya hili jambo kwa dhati litaleta mjadala  mpana hakuna mabadiliko yanayotokea kabla ya watu hawajaelimika na vyombo vya habari haviwafundishi watu kufikiri lakini vinawapa  suala la kufikilia.” alisema Mkurugenzi huyo wa UTPC.

Alisema, vyombo vya habari vitangalia sheria zilizopo iwapo zina kutosha na zinafanya kazi ,  kufanya uchambuzi na uchunguzi ili kubaini mapungufu yaliyopo  kwa lengo la kusaidia kupiga hatua .

“ Kikubwa vyombo vya  habari hatupendi kuona hatua zinachukuliwa baada ya tukio kutokea ,tunalo jukumu sisi  waandishi wa habari kutoa elimu ili kuzuia matukio yasitokee,  watu wanasema kuzuia ni bora kuliko kuponya “ alisisitiza  Simbaya.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa UTPC, Mjumbe wa Bodi hiyo ,Lilian Lucas,alisema waandishi wa habari  wanalo jukumu la kuwa mstari wa mbele la kuwasemea wanawake na watoto ambalo ndio kundi kubwa linaloathirika na vitendo vya  ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake mwandishi wa habari kutoka Klabu ya waandisdhi wa habari Zanzibar, Mwashabani Seif ,alisema Zanzibar kama sehemu ya Tanzania  ,watahakikisha watapaza sauti kwa kushirikiana na UTPC ili kuondokana na janga hilo .

UTPC itatumia siku  16 za kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kutoa elimu kwa  kuandaa mada na mijadala mbalimbali ikiwemo ndoa na mimba za utotoni, ukeketaji na vitendo vingine vyenye kuleta  madhara makubwa kwa jamii  na  hata kugharimu maisha ya watu.

Mwisho.

Habari Zifananazo

Back to top button