UVCCM waonywa uchaguzi wa kunyenyekewa

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV-CCM) umewataka wanachama wake kutochagua viongozi kwa kuangalia urafiki na undugu, bali wachague viongozi bora wa kukivusha chama katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Akizungumza jana kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Dodoma jana, Katibu wa UVCCM Taifa, Kenani Kihongosi alihimiza vijana wachague viongozi ambao hawatawagharimu kwa kipindi cha miaka mitano kwa kunyenyekea watu badala ya chama.

“Tuchague viongozi ambao hawataenda kufanya mambo kinyume na kanuni yetu ya Umoja wa Vijana. Msichaguane kwa urafiki, undugu…nendeni mkachague kiongozi bora ambaye mwaka 2024 tutavuka uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka 2025 tutavuka Uchaguzi Mkuu kwa kushinda kata na majimbo yote ya Dodoma,” alisema Katibu Mkuu wa UVCCM.

Aliongeza, “Msichague kiongozi mmbea, mtoa rushwa, mfitini, anayejali vitu visivyo vya msingi, leo ukichagua kesho usinung’unike tusipoyasema haya tutakuwa wanafiki.

“Tunaochagua kiongozi tujue tunachagua mtu wa kutuongoza kwa miaka mitano, tukichagua vizuri tutakwenda vizuri, mkichagua vibaya maamuzi mnayo nyie. Uhuru wa kuchagua wa kwenu, lakini mtuletee viongozi bora, imara, madhubuti, wenye hofu ya Mungu.

Aliwataka kuchagua viongozi watakaokwenda kusaidia kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na sio watu watakaokwenda kufanya kazi kwa maslahi yao.

“Twendeni tukachague watu ambao watakaokuwa wanyenyekevu na si wanyenyekevu ndani ya watu, ndani ya CCM. Mkifanya hivyo mtakwenda kukitendea haki chama, kumtendea haki Rais (Mwenyekiti wa CCM Taifa) wetu na vijana wa nchi hii,” alisema Kihongosi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button